Kenya,Nigeria na Afrika Kusini Magazetini | Magazetini | DW | 17.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Kenya,Nigeria na Afrika Kusini Magazetini

Uamuzi wa Kenya kuutaka Umoja wa mataifa uifunge kambi kubwa ya kimataifa ya wakimbizi ya Dadaab sawa na hali nchini Nigeria ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii

default

Kambi ya wakimbizi ya Dadaab,mashariki ya Kenya

Kenya imegonga vichwa vya habari vya magazeti na majarida ya Ujerumani wiki hii kutokana na uamuzi wake wa kuutaka Umoja wa mataifa uwaondowe wakimbizi wa kisomali toka kambi ya Dadaab katika kipindi cha miezi mitatu inayokuja,Nigeria pia imezingatiwa kutokana na ushindi wa upande wa upinzani katika uchaguzi wa majimbo na pia kutokana na kumbukumbu za mwaka mmoja tangu walipotekwa nyara na wanamgambo wa itikadi kali Boko Haram, wanafunzi wa kike toka mji wa Chibok ambao zaidi ya 200 hawajulikani waliko na pia hisia za chuki dhidi ya wageni nchini Afrika kusini.

"Kenya inataka kuifunga kambi kubwa kabisa ya wakimbizi ulimwenguni","uhamaji uliopangwa" au "kwasababu ya Hofu ya wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam" ni miongoni mwa vichwa vya habari vya ripoti za magazeti na majarida ya Ujerumani kuhusu uamuzi wa Kenya kutaka kambi ya Dadaab ifungwe haraka.Jarida la Der Stern linalozungumzia kuhusu "uhamaji uliopangwa",linatoa picha ya kambi hiyo na kusema aliyeiona mara moja tu hatoisahau milele picha aliyoipata.Safu zisizokuwa na mwisho za mahema,vibanda vilivyoezekwa kwa matawi ya miti na mikoba ya plastiki,nyumba za matofali ya rangi ya kahawiya,na mavumbi ya rangi nyekundu yaliyoenea kila pembe."Dadaab ni kambi kubwa kabisa ya wakimbizi ulimwenguni" linaandika der Stern linalokadiria wakimbizi wa kisomali kati ya laki tatu na nusu na laki nne wanaishi katika kambi hiyo iliyoko mashariki ya Kenya.Wiki moja baada ya magaidi wa Al Shabab kukivamia chuo kikuu cha Garissa na kuwauwa zaidi ya watu 150,serikali ya Kenya imetangaza kuifunga kambi hiyo.Magaidi walioingia Garisa wanatuhumiwa wanatokea Dadaab. Umoja wa mataifa na mashirika ya misaada ya kiutu wamepewa muda wa miezi mitatu kuwahamisha wakimbizi hao,la sivyo jeshi la Kenya litafanya hivyo.Der Stern linahisi Dadaab imeshaiponyoka serikali ya Kenya-wanamgambo wa kisomali ndio wanaoidhibiti hali ya mambo.Katika baadhi ya maeneo ya kambi hiyo,watumishi wa mashirika ya misaada hawawezi kuinia bila ya kufuatwa na watu wenye silaha.Hata hivyo Dadaab sio tena kambi ya muda iliyojengwa mwaka 1991-imegeuka mji,yakikutikana masoko inakouzwa sukari ya magendo sawa na simu za magendo za mkononi,petroli,biya, tambi au hata bunduki kichini chini.Na kila wiki mahema hugeuzwa nyumba za matofali ya kahawia.Mara kadhaa serikali ya Nairobi imetangaza kutaka kuifunga kambi hiyo,hadi wakati huu hakuna kilichofanyika,linamaliza kuandika jarida la der Stern.

Aibu kwa serikali kushindwa kuwaokoa wasichana wa Chibok

Nigeria Proteste Chibok Mädchen

Maandamano kudai wasichana wa Chibok wakombolewe

Nigeria pa imegonga vichwa vya habari vya ripoti za magazeti na majarida ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.Lilikuwa gazeti la "Süddeutsche Zeitung" lililoandika uhariri kuhusu kutekwa nyara na wafuasi wa itikadi kali wa Boko Haram mwaka jana na kutojulikana waliko mpaka leo, wanafunzi zaidi ya 200 wa kike katika shule yao ya Chibok."Kushindwa kwa aibu" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo la kusini mwa Ujerumani linalohisi pengine baadhi ya wasichana 219 waliosalia wameozeshwa kwa nguvu na wengine wamelazimishwa kuyatoa mhanga maisha yao kwa kujiripua.Pekee tangu mapema mwaka 2014,linaandika Süddeutshe Zeitung, likinukuu shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International,wasichana na akinamama wasiopungua 2000 wametekwa nyara na idadi ya waliouliwa katika kipindi hicho hicho inafikia watu 5500.Kisa cha Chibok ni kimoja tu kati ya vingi nchini Nigeria linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche linaloilaumu serikali kwa kushindwa kwa aibu kupambana na ugaidi.Ushindi wa upande wa upinzani katika chaguzi za rais na bunge nchini Nigeria nao pia umechambuliwa.Gazeti la mjini Berlin,die Tageszeitung linahisi ushindi huo unaweza kugeuka kizungumkuti kwakua majimbo yote ya mafuta katika eneo la Niger-Delta yamesalia mikononi mwa chama tawala cha zaidi PDP,hali inayoweza kuzusha uhasama wa kisiasa kati ya serikali kuu mjini Abuja na mji mkuu wa kiuchumi Lagos.

Malawi yawahamisha raia wake Afrika kusini

Südafrika Fremdenfeindliche Ausschreitungen

Machafuko dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusiki

Hatimae lilikuwa gazeti la frankfurter Allgemeine lililozungumzia kuhusu chuki dhidi ya wageni nchini Afrika kusini chuki zilizopelekea Malawi kuangaza kwarejesha nyumba raia wake 400 wanaoishi katika nchi hiyo jirani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL /presse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com