1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yazindua reli nyingine mpya ya kisasa SGR

Wakio Mbogho18 Januari 2022

Kenya imeuzindua rasmi uchukuzi wa reli nchini na kimataifa baada ya kukamilisha uunganishaji wa reli mpya ya kisasa SGR na reli ya zamani iliyokarabatiwa.

https://p.dw.com/p/45fzD
Kenia Standard Gauge Railway in Kimuka
Picha: Reuters/T. Mukoya

Akizungumza mjini Naivasha baada ya kushuhudia rasmi ukamilishaji wa kuunganisha reli ya kisasa ya SGR na reli ya zamani, mkurugenzi mkuu wa shirika la reli la Kenya Philip Mainga amesema hatua hiyo inadhihirisha namna teknolojia ya kisasa inaweza kuboresha uchukuzi.

"Mfumo huu wa reli umeunganishwa kutoka hapa, hadi Malaba na Kampala. Kile kitakachokuwa kinafanyika hapa, badala ya kuyashusha makasha chini yakifika hapa, mfumo huu utatumika kutoa mzigo kutoka eneo moja au reli moja hadi nyingine bila kugusa ardhi"

Kenia Nairobi SGR Güterzug
Kituo kikuu cha treni cha NairobiPicha: Reuters/T. Mukoya

Bandari kavu iliyojengwa mjini Naivasha ambayo hutumika kuhifadhia mizigo, inaunganisha bandari ya Mombasa na magharibi mwa Kenya na sasa itakuwa kitovu cha usafirishaji mizigo nchini na kwa mataifa mengine ya Afrika. Hii ni mara ya kwanza baada ya zaidi ya muongo mmoja kwa Kenya kufanikiwa kupunguza muda wa kusafirisha mizigo kutoka Mombasa hadi Malaba mpakani mwa Kenya na Uganda.

"Awali tulipokuwa tunatumia ile reli ya zamani, ilikuwa inatuchukua siku tatu au nne kufika mpaka wa Malaba. Tumepunguza hiyo hadi saa 26 au 28. Tumepunguza pia safari ya Kampala, Uganda kutoka siku saba hadi saa 36"

Mradi huu unawalenga wafanyibiashara, wakulima na wamiliki wa viwanda wanaosafirisha mizigo yao, kwa kuwa bei ya uchukuzi kutumia reli imepunguzwa mara dufu. Wakenya wameukaribisha uzinduzi wa mradi huo wa uchukuzi kwa maoni tofauti.

Siku chache zilizopita, Rais Uhuru Kenyatta alifanya ziara ya ghafla ya kukagua bandari ya Kisumu inayoendelea kujengwa na ambayo itafaidika pakubwa kutokana na mfumo huu wa reli.