1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yashuka zaidi katika nchi zisizoweza kukopesheka

10 Julai 2024

Rais wa Kenya William Ruto ametahadharisha kuwa hatua ya kuukataa mswada wa fedha wa mwaka 2024 itakuwa na athari kubwa kwa taifa hilo lenye uchumi mkubwa katika kanda ya Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/4i6J6
Kenya I Rais Ruto baada ya maandamano ya kupinga nyongeza ya kodi
Rais wa Kenya William RutoPicha: Patrick Ngugi/AP/picture-alliance

Deni kubwa la nchi hiyo linatarajiwa kuongezeka zaidi baada ya maandamano yaliyompelekea Rais Ruto kuufutilia mbali mswada huo. Haya yanafanyika wakati ambapo Kenya imeshushwa katika kiwango kimoja zaidi katika orodha ya mataifa yasiyoweza kukopesheka.

Akiwa anakabiliwa na miito ya kujiuzulu, Rais William Ruto amesema kwamba serikali itageukia kuipunguza kwa nusu, nakisi ya bajeti ya dola bilioni 2.7 kisha igeukie kukopa kiasi kitakachosalia bila kusema atakokopa fedha hizo.

Kenya kwa sasa ina deni la dola bilioni 80 kutoka kwa mashirika ya ukopeshaji kama Benki ya Dunia, Shirika la fedha Duniani IMF na China. Jinsi utawala wa Ruto utakavyozipata fedha za kulipa deni hilo bila kuwaghadhabisha zaidi Wakenya ambao wanakabiliwa na ugumu wa maisha na bila kuipunguza kasi ya ukuaji wa uchumi, ndilo swali kuu.

Kenya haiwezi tena kukopesheka

Haya yanafanyika wakati ambapo taasisi ya kimataifa ya kutathmini viwango vya ukopeshaji ya Moody imeishusha Kenya na kuiorodhesha katika viwango vya chini zaidi vya taifa lisiloweza kukopesheka.

Taasisi hiyo imetahadharisha kwamba hali ya taifa hilo ni mbaya, baada ya wimbi la maandamano kuilazimisha serikali mjini Nairobi kuitupilia mbali mipango ya nyongeza ya kodi.

Waandamanaji Kenya ´wamkalia kooni´ Ruto

Taasisi hiyo yenye makao yake nchini Marekani, imesema inateremsha viwango vya uwezo wa Kenya kukopesheka kwa hatua moja chini, hali ambayo inatazamwa kama kitisho kikubwa kwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kuhusiana na uwezo wa kupata mkopo.

Tathmini hiyo mpya  ya taasisi ya Moody huenda ikaitumbukiza Kenya katika nafasi ya kukabiliwa na gharama kubwa ya ulipiaji madeni yake kwani hii inamaanisha kwamba Kenya italipa madeni yake kwa riba ya juu zaidi.

Mbui Wagacha ni mchumi ambaye pia alikuwa mshauri wa zamani wa rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta na anasema iwapo nchi hiyo itakopa zaidi, basi hilo ni jambo linaloweza kuitumbukiza nchi katika matatizo zaidi. Wagacha anapendekeza mkakati wa kutumia diplomasia kwa ajili ya kuvutia uwekezaji na kuliangazia upya deni la nchi hiyo ili kuwashawishi  wakopeshaji wafutilie mbali sehemu ya deni hilo.

IMF ilipendekeza nyongeza ya kodi

Mchumi mwengine Ken Gichiga amekiri kwamba iwapo Kenya itakopa zaidi basi kasi ya ukuaji wa uchumi wake itarudi chini, kwani biashara bado hazijafufuka kutokana na athari za janga la Uviko-19 na vita vya nchini Ukraine.

Deni la Kenya ni asilimia sabini ya pato jumla la nchi hiyo, hicho kikiwa ndicho kiwango cha juu zaidi cha deni kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miaka 20.

Shirika la fedha duniani IMF lilipendekeza baadhi ya nyongeza za kodi zilizopelekea maandamano nchini humo, na lilionekana kulengwa na baadhi ya waandamanaji wiki mbili zilizopita, huku wengine wakionekana na mabango yaliyoandikwa, "IMF wacheni ukoloni."

Maandamano dhidi ya nyongeza ya kodi Nakuru
Waandamanaji Nakuru wakiwa na mabango ya kuilaumu Benki ya DuniaPicha: James Wakibia/SOPA Images/IMAGO

Katika taarifa IMF ilisema kwamba inaitazama hali inavyoendelea nchini Kenya na kwamba lengo lake ni kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na changamoto za kiuchumi inazokabiliana nazo na kuwasaidia watu wake waishi maisha bora.

Vyanzo: AP/AFP