Kenya yarefusha marufuku ya usiku wakati shule zikifunguliwa | Matukio ya Afrika | DW | 04.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kenya yarefusha marufuku ya usiku wakati shule zikifunguliwa

Kenya imeongeza muda wa utekelezaji wa hatua za kukabiliana na virusi vya Corona hadi Machi 12 mwaka huu, huku shule zote nchini humo zikifunguliwa kwa mara ya kwanza tangu kufungwa mwezi Machi mwaka uliopita.

Hatua hizo ni pamoja na marufuku ya kutoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi asubuhi. Aidha maeneo ya burudani yatahitajika kufungwa ifikapo saa tatu usiku kama alivyoagiza Rais Uhuru Kenyatta. Awali maeneo hayo yalikuwa yakifungwa saa nne usiku. Huku akikiri kuwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona vinaendelea kupungua, rais Kenyatta alibainisha kuwa janga hilo linasalia kuwa kitisho kwa taifa. Mwezi Novemba, rais alikuwa ameongeza muda wa hatua hizo hadi tarehe tatu Januari. Waziri wa Usalama wa Taifa dokta Fred Matiang'I alisoma agizo hilo.

"Mheshimiwa rais, ametoa agizo kuu, akiongeza muda wa baadhi ya masharti, kuhakikisha kuwa wanafunzi wanarejea katika mazingira salama shuleni. Hivyo ameongeza muda wa kafiu.”

Kwenye agizo hilo, mikutano ya kidini ama sherehe za harusi na mazishi, wahusika watahitajika kuzingatia masharti yaliyotolewa na baraza la viongozi wa dini mbali mbali nchini. Watu 150 pekee ndio watakaoruhusiwa kuhudhuria hafla za mazishi. Mikutano ya siasa ingali imepigwa marufuku kwa siku 60 zijazo. Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakionekana kuandaa mikutano hiyo ama kupigia debe ripoti ya maridhiano ya BBI au wengine wakiipinga.

Kenia Nairobi Coronavirus Ausgangssperre Patrouille Kontrolle

Wanajeshi katika doria ya kutotembea usiku

Ujio wa marufuku ya kutembea usiku ni changamoto kwa wazazi ambao wanahitajika kuwalipia watoto wao ada za shule, huku serikali ikirejesha kodi kwa hudumu kadhaa ilizokuwa imeondoa mwaka uliopita. Ili kuwalinda wanafunzi shule zinapofunguliwa, rais ameagiza walimu na wafanyikazi wengine shuleni walio na zaidi ya umri wa miaka 58, kutekeleza majukumu yao kupitia mtandao. Serikali imeahidi kutoa barakoa kwa wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuzinunua kama anavyofafanua Daktari George Magoha,  waziri wa elimu.

”Serikali itatoa madawati 500,000 kwa shule, kuhusu suala la barakoa, hatuna mjadala, kwa kuwa wanafunzi wote watakaoingia shuleni watapewa.”

Shule zimetakiwa kuhakikisha kuwa zina vifaa vya kutosha vya kukabiliana na janga la corona kwa mujibu wa muongozo wa Wizara ya Afya. Michezo ya shuleni kama vile uigizaji, muziki, kandanda na hafla za kuwatuza wanafunzi zawadi, vimepigwa marufuku kwa kipindi cha siku 90. Daktari Magoha amesema kuwa ana Imani kuwa wanafunzi watafidiwa muda waliopoteza shule zilipokuwa zimefungwa. Kufunguliwa kwa shule ni mwanzo wa muhula wa pili, ambao unatarajiwa kukamilika katikati ya mwezi Machi mwaka huu.