1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Watu 13 wauwawa wakiwemo watoto sita

Mwakideu, Alex3 Machi 2008

Watu 13 wauwawa nchini Kenya katika ghasia za kupigania ardhi

https://p.dw.com/p/DHIB
Kibaki na Raila watia sahihi makubaliano ya kuunda serikali ya muungano.Picha: picture-alliance/ dpa

Huku wanasiasa nchini Kenya wakiahidi kuharakisha mazungumzo kuhusu ardhi na rasilmali, watu 13 wameripotiwa kuuwawa magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika mashariki.


Polisi wanasema kundi watu waliojihami kwa bastola na mapanga walivamia kijiji kimoja katika jimbo la magharibi mwa Kenya na kutumia risasi, mapanga na kuchoma nyumba.


Mkuu wa polisi katika mkoa wa magharibi Bernard Muli ametaja mwanamke mja mzito na watoto wengine sita kuwa miongoni mwa wale waliofariki.


Msemaji wa polisi nchini Kenya Eric Kiraithe amesema mauaji hayo katika eneo lililoko kilomita 500 kaskazini magharibi mwa Nairobi yanahusiana na maswala ya ardhi na wala sio uchaguzi wa disemba 27.


Mmoja wa waathirika Rabson Mbuya ameelezea kwamba mkewe, watoto wake watatu na mfanyikazi wa nyumbani waliuwawa katika uvamizi huo baada ya nyumba yake kuchomwa akitizama.


Wakati huo huo wanasiasa nchini Kenya wameapa kuharakisha mazungumzo kuhusu ardhi na rasilmali; baadhi ya sababu zilizopelekea ghasia baada ya uchaguzi wa disemba 27


Wakenya ambao walikuwa wamechoshwa na visa vya wizi, uchomwaji wa mali na mauaji waliukaribisha mpango mpya wa serikali inayoshirikisha upinzani uliotiwa sahihi wiki jana.


Katibu mkuu wa zamani Koffi Annan ambaye aliongoza makubaliano hayo aliwaomba wakenya waunge mkono mpango huo mpya na waungane na viongozi wao hadi pale watakapofaulu kikamilifu kutatua maswala ya ardhi na uchaguzi.


Annan ambaye aliondoka nchini humo na kumuachia uongozi waziri wa zamani wa mambo ya nje huko Nigeria Oluyemi Adeniji alisema maswala tata zaidi yanapaswa kutatuliwa katika kipindi cha mwaka mmoja. Hata hivyo wawakilishi wa PNU na ODM katika mazungumzo ya upatanishi walionyesha matumaini ya kutafuta utatuzi wa kudumu katika kipindi kifupi zaidi.


Baada ya kikao cha kwanza ambacho kilisimamiwa na Adeniji, mwakilishi wa serikali katika mazungumzo hayo Mutula Kilonzo amesema wanatajia wataweza kutatua maswala hayo wiki hii.


Musalia Mudavadi ambaye anawakilisha upinzani amesema hatarajii maswala yaliyobakia yajadiliwe kwa mwaka mzima na kwamba watatafuta njia za kuharakisha mazungumzo hayo.


Bunge linatarajiwa kufunguliwa alhamisi na kupasisha marekebisho ya katiba ambayo yatawezesha kuundwa kwa serikali ya muungano itakayoongozwa na Rais Mwai Kibaki huku mpinzani wake Raila Odinga akitengewa nafasi mpya ya waziri mkuu.


Zaidi ya watu 1000 waliuwawa na wengine 300, 000 wakaachwa bila makao baada ya ghasia kuikumba Kenya punde tuu Rais Kibaki alipotangazwa mshindi katika uchaguzi ambao mpinzani wake Odinga anasema ulikumbwa na udanganyifu.


Ghasia hizo zilitarajiwa kuipotezea Kenya dola bilioni 3.8 katika kipindi cha nusu mwaka kulingana na muungano wa watengenezaji wa Kenya.


Marekani ambayo ilimtuma waziri wake wa nchi za nje Condoleezza Rice nchini humo akatilie mkazo mazungumzo yaliyokuwa yakiendeshwa na Koffi Annan imetoa msaada wa dola milioni 14. 7 kama msaada kwa Kenya.


Licha ya wakenya wengi kufurahia makubaliano kati ya Odinga na Kibaki, wengine wangali wanatilia shauku uwezekano wa viongozi hao wa kufanya kazi kwa pamoja kama Rais na waziri mkuu haswa baada ya madai kwamba Kibaki alipuuza makubaliano ya mwaka wa 2002 yaliyokuwa yananuia kutengeneza nafasi ya waziri mkuu kwa Odinga.