Kenya na Uganda kuzindua kituo cha pamoja mpakani Busia | Matukio ya Afrika | DW | 24.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kenya na Uganda kuzindua kituo cha pamoja mpakani Busia

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni wanajumuika pamoja leo Jumamosi kwa hafla maalum ya uzinduzi rasmi wa kituo cha pamoja cha kutoa huduma za mpakani baina ya Kenya na Uganda, mjini Busia.

 Uzinduzi wa kituo hicho ni mojawapo ya hatua za kurahisisha biashara na uhamiaji miongoni mwa raia wa nchi zote mbili, chini ya mchakato wa kutekeleza itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashiriki. Vituo vingine kama hivyo vimejengwa kwenye mipaka ya nchi hizo na Tanzania pamoja na Rwanda.

Marais Uhuru Kenyatta na Yoweri Museveni watakariri umuhimu wa kuondoa urasimu ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika kwa utaratibu tena kwa ufanisi zaidi.

East African Community EAC Eriya Kategaya Ostafrikanische Gemeinschaft (AP)

Uzinduzi wa soko la pamoja la Afrika Mashariki

Florence Atieno ambaye ni mwenyekiti wa kundi la wanawake wafanyabiashara wadogo wadogo wa eneo la mpakani la Busiaanasema kabla ya kupata huduma hiyo mpya wafanya biashara walikuwa wanakabiliwa na changa moto chungu nzima.

''Hapo awali sisi kama wafanya biashara wa mpakani tulikumbana na changa moto si haba. Wengi walikuwa wanatumia njia za mkato na hivyo kupatana na masaibu chungu nzima kama vile wanawake kubakwa, kupoteza mizigo na hata watoto. Lakini kwa sasa, mambo yamebadilika. Kutokana na kituo hiki cha pamoja, gharama ya kufanyia biashara imepungua na tunapata faida. Pia usalama wetu umeimarika''. Amesema Florence Atieno.

Busia ni kivukio muhimu kwa wafanya biashara wa mataifa ya kanda ya Afrika Mashariki. Mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha pamoja kimefadhiliwa kwa kima cha zaidi ya dola milioni 12 kupitia shirika la mpango wa maendeleo la Uingereza, DFID, kwa ushirikiano na serikali ya Canada.  


Mwandishi: Reuben Kyama 
Mhariri: Caro Robi