1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Mzozo wafukuta kuhusu msitu wa Mau

Wakio Mbogo4 Septemba 2019

Chama cha mawakili nchini Kenya kimeomba kujumuishwa katika kesi inayohusu mpango wa serikali kuwafurusha watu kutoka msitu wa Mau ili kuuhifadhi. Serikali na wanasiasa wanazozana kuhusu uamuzi wa kuwaondoa wavamizi.

https://p.dw.com/p/3P0fz
Afrika ethnischen Gruppe der Ogiek
Picha: Getty Images/AFP/R. Schmidt

Chama cha kitaifa cha mawakili nchini Kenya, LSK, kimewasilisha ombi la kutaka wajumuishwe kwenye kesi inayohusu mpango wa serikali kuwafurusha watu kutoka msitu wa Mau.

Ingawa wanaunga mkono mpango wa serikali wa kuuhifadhi msitu huo, wanasema wanataka kuisaidia mahakama kuelewa sera na sheria zinazohusu mazingira, ardhi na haki za kibinadamu.

Wakili Kipng'eno Ngetich mwanachama wa LSK ameshauri zoezi la kuwafurusha watu lisitishwe ili kutoa nafasi kwa swala hili kushughulikiwa kisheria na ndiyo maana wameenda mahakamani kutaka muongozo wa kisheria.

Katika awamu hii ya pili serikali inapanga kuziondoa takriban familia elfu 60 kutoka msitu Mau lakini mchakato huo umeibua vuta ni kuvute wengi wa wakaazi wa eneo hili wakisisitiza wana hati halali za umiliki wa ardhi wanamoishi.

Afrika ethnischen Gruppe der Ogiek
Wanakiji wa Kenya wakisimama karibu na shamba lililolimwa kwenye kilima ambacho kilikuwa sehemu ya msitu wa Mau,ambao ni muhimu kwa upatikanaji wa maji kwa sehemu kubwa ya Kenya.Picha: Getty Images/AFP/R. Schmidt

Maelewano hakuna

Kiongozi wa maseneta walio wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen amemkosoa waziri wa ardhi Keriako Tobiko kwa kuyakaidi mamlaka ya rais na kuwalazimishia ajenda yake anayosema sio halali. Murkomen anadai baraza la mawaziri halijapitisha maafikiano hayo.

Tayari baadhi ya watu wameshaanza kuondoka kutoka maakazi yao huko msitu Mau huku serikali ikiwapa muda wa siku 60 kuondoka kwa hiari kuepuka kuondolewa kwa nguvu makataa hiyo itakapoisha.

Wakili Kipng'eno Ngetich vilevile anahoji kuwa maeneo ya Narok yanayoangaziwa huenda iwe ardhi ya ujumla ya jamii na ipo haja ya kuwahusisha wasoroveya kutoa mwelekeo hususan. Anashauri zoezi hilo lifanywe kwa kuzishirikisha asasi zote zinazohusika.

Serikali ya Kenya imebatilisha agizo lake la kuzifunga shule zilizoko eneo hilo la mau hadi mwezi ujao wanadunzi watakapokamilisha mitihani yao ya kitaifa.

Chanzo: DW Nakuru