Kenya kuongoza msukumo wa vuguvugu la Pan African | Matukio ya Afrika | DW | 12.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kenya kuongoza msukumo wa vuguvugu la Pan African

Kenya imeahidi kuongoza msukumo wa vuguvugu la Pan-African ili kuiwezesha Afrika kuendesha agenda yake ya maendeleo kwa njia huru. Hayo yamesemwa mjini Nairobi kwenye kongamano la siku tatu la Eneo la Afrika Mashariki

Kuondolewa kwa mipaka ya ukoloni ni moja ya maazimio yaliyotolewa kwenye kongamano hilo. Wajumbe wa Vuguvugu hilo la Pan Africanism wamesema kwamba mipaka ya ukoloni ilichorwa bila waafrika wenyewe kushauriwa na kwamba uhuru unaombatana na umasikini si uhuru na hivyo waafrika wanao uwezo wa kujiamulia hatika yao. Rais Uhuru Kenyatta kwenye hotuba yake ya kufungwa kwa kongamano la Afrika Mashariki la Vuguvugu la Pan African Movement amesema…“Kuwepo kwa Afrika iliyo huru kisiasa, kiuchumi pamoja na idadi yake kubwa ya vijana na uhuru wa kufanya biashara na kutenbea bila shaka utalifanya bara la afrika kuongoza dunia nzima”

Waziri wa haki na maswala ya katiba nchini Uganda Meja Generali Kahinda Otafiire amesoma maazimio ya kongamano hilo ambayo yalikuwa ni pamoja na kuondolew kwa mipaka ya kikoloni katika mataifa ya Bara la Afrika.

“Tungeomba kupendekeza kwamba mpaka wa mangharibi mwa Kenya uwe Dakar, mpaka wa kusini mwa Kenya uwe Cape Town na mpaka wa kaskazini uwe Alexandria. Na ningependa kuipa Jamhuri ya Kenya jina jipya iitwe Jamhuri ya Afrika”

Meja Generali Kahinda amesema wazungu waliwaganya waafrika ili ilwe rahisi kwao kuwatawala. “Hii swala la Francophone, Anglophone, sijui phone gani. Tunataka kuwa Africaphone. Tunataka kuzungumza kwa niaba ya watu wa Afrika na kwa ajili yetu”.

kuondolewa kwa visa za kitalii kwa Waafrika wanaozuru nchi za Afrika ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa kwenye kongamano hilo. Kongamano hilo limehudhuriwa na Waakilishi kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki, Ethiopia, Eritrea, Sudan Kusini, Somalia na Djibouti.

Botswana imeandaa kongamano la Pan Africa Congress kwa ajili ya tawi la eneo la Afrika Kusini, Congo nayo inaandaa kikao kwa niaba ya Afrika ya kati huku Afrika Magharibi ikiwakilishwa na Ghana kwenye kikao kilichoandaliwa sambamba haoa Nairobi.

Vikao hivyo vimeandaliwa mbele ya kongamano la 9 la vuguvugu la Pan African litakalofanyika mwaka ujao. Pan Africanism ni msukumo wa vuguvugu la Waafrika unaohimiza umoja wa Waafrika kote duniani. Msukumo huo unazingatia imani kwamba umoja ni muhimu kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi kisiasa na kijamii na unalenga kuwaleta pamoja na kuinua maisha ya waafrika.

Mwandishi:Alfred Kiti
Mhariri:Josephat Charo