1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: IEBC yakanusha madai ya udukuzi

10 Agosti 2017

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya, Ezra Chiloba, amepinga madai yaliyotolewa na upinzani nchini humo kuwa matokeo ya uchaguzi wa rais yamedukuliwa. Ni kinyume na madai ya Raila Odinga.

https://p.dw.com/p/2hyfP
Wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi Kenya, IEBC
Picha: picture-alliance/dpa/F. Dlangamandla

Mgombea wa urais wa Muungano wa upinzani wa NASA amedai matokeo yanayotolewa na tume hiyo yanayoonyesha mgombea wa chama tawala Uhuru Kenyatta anaongoza ni ya uongo. Chiloba amewaambia waandishi wa habari kuwa mifumo ya tume hiyo ya uchaguzi iko salama na hakuna udukuzi wowote uliofanyika hapo kabla, wakati wa upigaji kura na hata baada ya upigaji kura kulingana na uchunguzi waliofanywa kufuatia malalamiko yaliyotolewa na upinzani ukidai kuna udukuzi uliofanyika katika mfumo wa kielektroniki wa tume hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) na Raila Odinga wa upinzani ni wagombea wakuu wa urais
Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) na Raila Odinga wa upinzani ni wagombea wakuu wa urais

Matokeo ya awali yaliyotolewa kupitia tovuti ya tume ya uchaguzi nchini Kenya yanamuonesha Rais Uhuru Kenyatta akiongoza kwa asilimia 53.3 kulingana na kura zilizokwisha hesabiwa hadi sasa huku mgombea wa muungano wa upinzani Raila Odinga akiwa na asilimia 44.8.Mapema Raila Odinga aliandika kupitia katika ukurasa wa twitter akisema kulingana na tathimini iliyofanywa na chama chake alikuwa akiongoza kwa kura milioni 8.1 dhidi ya kura milioni 7.2 za Uhuru Kenyatta. Hata hivyo hakutoa uthibitisho unaohusiana na matokeo hayo.Wakati huohuo duru kutoka nchini humo zinasema Polisi walilazimika kufyatua risasi na kuwaua watu watatu kufuatia maandamano yaliyofanyika katika maeneo kadhaa nchini humo ikiwa ni pamoja na katika mji wa Kisumu ambao ni ngome kuu ya mgombea wa upinzani.