Kenya hali bado sio shwari | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 01.01.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Kenya hali bado sio shwari

---

NAIROBI

Rais Mwai Kibaki wa Kenya amezidi kushinikizwa na nchi za magharibi kukubali pafanyike uchunguzi juu ya madai ya mizengwe katika uchaguzi mkuu uliozusha ghasia za kikabila nchini Kenya.

Umoja wa Ulaya katika ripoti yake ya mwanzo juu ya uchaguzi huo umeelezea shakashaka zake kuhusiana na zoezi zima lilivyoendeshwa.Kiongozi wa ujumbe wa umoja huo katika uchaguzi huo,bwana Alexander Lambsdorf amekosoa vikali jinsi uchaguzi ulivyokwenda akigusia zaidi namna matokeo ya urais yalivyokuwa yakitolewa.Waangalizi wamesema kulikuwa na dosari na uchaguzi wa rais haukufikia viwango vya kimataifa.Aidha Alexender Lambsdorf ameelezea kusikitishwa kwake na jinsi waangalizi wa kimataifa walivyokuwa wakizuiliwa kufanya kazi zao katika vituo mbali mbali vya kupigia kura na hata kuzuiliwa kuingia katika ukumbi wa kuhesabu kura.Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amewataka viongozi wote kuwa na umoja na kufanya mazungumzo ya kuleta maridhiano pamoja na kuunda serikali ya Umoja.

Anasema Ghasia lazima zikomeshwe nimezungumza na bwana Kibaki na pia bwana Odinga ninachotaka kukiona ni kuja pamoja kwa viongozi hawa kuwa na mazungumzo maridhiano na Umoja na pia nataka kuona uwezekano wa ikiwa wanaweza kuwa pamoja ndani ya serikali.’’

Hata hivyo Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga amesema atakuwa tayari kuwa na mazungumzo na rais Kibaki ikiwa tu atakubali kwamba alishindwa kwenye uchaguzi huo na kura zihesabiwe tena chini ya uangalizi wa kimataifa.Aidha bwana Odinga amethibitisha taarifa kwamba idadi ya waliokufa hadi sasa inaweza ikawa imefikia watu 250.

Lakini msemaji wa serikali Alfred Mutua amevikosoa vyombo vya habari vya kimataifa kwa madai ya kutoa taarifa zisizo sahihi akisema,

Kenya haijafikia kiwango cha kuteketea na wala haitafikia huko ingawa amekiri kuna maeneo machache yanayokumbwa na Ghasia.

Taarifa za hivi punde zilizotolewa na shirika la msalaba mwekundu zinasema watu kiasi cha 30 wameuwawa kwa kuchomwa moto ndani ya kanisa walilokimbilia kujihifadhi huko magharibi mwa nchi hiyo hii leo.Katika ghasia za hapo jana nyumba ya kifahari ya rais Mstaafu Daniel Arap Moi huko Koibatek pia ilitiwa moto. Polisi wanaendelea kushika doria katika miji ya Kisumu na Nairobi. Taarifa pia zinasema Polisi imekataa kutoa leseni kwa upinzani kufanya mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika alhamisi,ikidai mkutano huo utatishia hali ya usalama wa taifa.Kiongozi wa Upinzani wa chama cha ODM bwana Raila Odinga amewalaumu maafisa wa polisi kwa ghasia na mauaji ya watu yaliyotokea na kusema mkutano ulipangwa kufanyika katika uwanja wa Uhuru Park Jijini Nairobi alhamisi utaendelea kama ulivyopangwa licha ya marufuku iliyotolewa.

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com