1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha marubani KALPA chataka wakurugenzi kufutwa kazi

13 Oktoba 2016

Kitisho hicho tayari kimeanza kulitumbukiza shirika hilo kwenye hasara, kwani wateja ambao walishanunua tiketi wameanza kukatiza safari zao na kurudisha tiketi baada ya kuingiwa  na wasiwasi kwamba safari zao zitatatizwa

https://p.dw.com/p/2RBIl
Kenya Airways Flughafen Nairobi ARCHIV
Picha: picture-alliance/dpa

Shirika la ndege  la Kenya, Kenya Airways limesema litasitisha uuzaji wa tiketi za usafiri kwa abiria ikiwa marubani hawatafutilia mbali mgomo ambao wameuitisha kuanzia wiki ijayo . Tayari abiria ambao walishanunua tiketi za  shirika hilo wameanza kuzirudisha  wakihofia safari zao zitatatizwa na kitisho hicho cha mgomo. 

Chama cha  marubani wa shirika la ndege nchini Kenya KALPA, kimeitisha mgomo wa marubani wao wote kuanzia siku ya Jumanne wiki ijayo , kikilalamikia usimamizi na uongozi mbaya wa shirika la ndege la Kenya Airways.

Kitisho hicho tayari kimeanza kulitumbukiza shirika hilo kwenye hasara, kwani wateja ambao walishanunua tiketi wameanza kukatiza safari zao na kurudisha tiketi baada ya kuingiwa  na wasiwasi kwamba safari zao zitatatizwa. Kenya Airways ambalo asilimia 27 linamilikiwa na shirika la ndege la Uholanzi  KLM, na asilimia 30 kumilikiwa na serikali ya Kenya, limesema halitakuwa na budi kusitisha uuzaji wa tiketi zaidi ikiwa Chama cha KALPA hakitafutillia mbali tishio la mgomo huo.

Katika miaka ya hivi karibu, shirika la Kenya Airways ambalo husafirisha abiria elfu 12,000 kila siku kutumia ndege zao aina ya Boeing na EMbraer, limekumbwa na hasara za mapato kufuatia kupungua kwa idadi ya wageni wanaozuru Kenya.

Kenya Airways Boeing 737-800
Kenya Airways Boeing 737-800Picha: AP

Utalii umeyumbishwa kutokana na  wasiwasi uliopo kuhusu usalama kufuatia mashambulizi ya kundi la kigaidi la Alshabaab nchini Somalia lenye uhusiano na mtandao wa Alqaeda. Mashambulizi ambayo ni ya ulipizaji  kisasi kufuatia Kenya kutuma wanajeshi wake nchini Somalia kulikabili  kundi hilo, baada ya kutishia utalii wa Kenya.

Chama cha KALPA kilicho na takriban marubani 450 ambao ni wanachama wake, kinamtaka mkurugenzi mkuu wa shirika hilo  Mbuvi Ngunze na mwenyekiti balozi Dennis Awori kujiuzulu au wafutwe kazi, kikidai hakina imani kwa wawili hao kuongoza mchakato wa kulifufua shirika hilo.

Hata hivyo shirika la Kenya Airways limesema hakuna sababu ya kutosha kwa muungano wa KALPA kuitisha mgomo, huku likiongeza kuwa matokeo ya kibiashara ya nusu mwaka ambayo yanatarajiwa kutangazwa mwisho wa mwezi Oktoba yanaonesha kuwa idadi ya abiria wanaosafiri kwa ndege za shirika hilo imeongezeka kwa asilimia nne, na kufikia abiria milioni 2.23 huku ndege zao zikijaa kwa asilimia 71, na kuwa viwango vya hasara vimepungua kwa bilioni tano.

Shirika hilo limeongeza kuwa mgomo huo utasababisha wafadhili na washirika wengine wanaohusishwa kwenye mchakato wa kuliimarisha zaidi kupoteza imani . Shirika hilo linalojulikana pia kama KQ ambalo tayari limesema linahitaji shilingi bilioni sabini kama mtaji, lipo katika harakati za kupunguza idadi ya ndege zake, idadi ya wafanyakazi, kando na kuuza ardhi na mali zake nyingine kama hatua ya kujinasua kwenye  hasara baada ya idadi ya watalii kupungua.

Mwandishi: John Juma/RTRE

Mhariri: Yusuf Saumu