1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kemboi kuhudumu katika tume ya wanariadha

27 Novemba 2015

Bingwa wa ulimwengu na Olimpiki katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Mkenya Ezekiel Kemboi ameteuliwa katika Tume ya wanariadha ya IAAF

https://p.dw.com/p/1HDkn
Olympia London 2012 3000 Meter Hindernis
Picha: Reuters

Kemboi, mwanariadha pekee kushinda mataji matatu ya ulimwengu katika mbio za mita 3,000, anaungana na mwanariadha mwanamke anayeshikilia rekodi ya ulimwengu ya marathon Muingereza Paula Radcliffe miongoni mwa wengine katika tume hiyo yenye wanachama 18 kuanzia mwaka wa 2016 hadi 2019.

Kemboi mwenye umri wa miaka 33 anayepanga kustaafu baada ya michezo ya mwaka ujao ya Olimpiki mjini Rio amesema ni heshima kubwa kwake na analenga kuitumia katika kupigania haki za wanariadha. Tume hiyo inatarajiwa kumchagua mwenyekiti mpya kuchukua nafasi ya nguli wa riadha Mnamibia Frankie Fredricks, atakaeyeendelea kuhudumu katika wadhifa wa heshima.

China Beijing 2015 IAAF Weltmeisterschaft Genzebe Dibaba
Genzebe DibabaPicha: picture-alliance/dpa/S. Suki

Dibaba mwanariadha bora mwanamke ulimwenguni

Kwinginikeo, mwanariadha wa Ethiopia Genzebe Dibaba ameshinda tuzo ya Mwanariadha Bora wa Mwaka ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kwa upande wa wanawake.

Dibaba ameshinda tuzo hiyo baada ya kuvunja rekodi za dunia katika mbio za 1,500 nje ya ukumbi, mita 5,000 ndani ya ukumbi na kwa kutwaa dhahabu ya mita 1,500 katika mashindano ya ubingwa wa riadha duniani mjini Beijing.

Tanzania kuwafanyia wanariadha vipimo

Shirikisho la riadha nchini Tanzania – AT linasema litafanya vipimo vya lazima kwa mara ya kwanza vya dawa za kusisimua misuli, wakati wa mashindano yajayo ya Kilimanjaro International Marathon yatakayoandaliwa mjini Moshi mnamo Februari 28 mwaka ujao.

Katibu mkuu wa AT Bibi Ombeni Mzavara amesema shirikisho hilo limekubaliana kufanya vipimo hivyo kutokana na kilio cha jumuiya ya kimataifa kuhusu matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu miongoni mwa wanariadha. Aidha amesema AT itatoa mapendekezo ya kuzuia au kudhibiti matumizi ya dawa hizo katika riadha.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/reuters
Mhariri: Josephat Charo