Kazi imeanza, Ujerumani yataka kuimarisha sera yake ya nje | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kazi imeanza, Ujerumani yataka kuimarisha sera yake ya nje

Ziara ya kwanza ya waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle na waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel, Afrika ni hatua ya kwanza inayoonyesha sera ya nje ya Ujerumani katika siku za usoni itaimarika

default

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle

"Kuna mambo kadhaa yanayopasa kufanyika katika siasa ya Ujerumani, kabla sera yake ya nje kuimarika," anasema mwandishi wetu, Ute Schäeffer, mkuu wa idara ya Afrika na Mashariki ya Kati ya Deutsche Welle hapa mjini Bonn.

Sio tu tangu kufanyika uchaguzi wa mwezi Septemba mwaka jana 2009 nchini Ujerumani, ambapo juhudi zimekuwa zikifanyika kuanisha lengo muhimu la kisiasa linalotoa mtizamo wa Ujerumani katika nchi za nje, hususan katika masuala ya kidiplomasia, utamaduni wa sera zake za kigeni, mausala ya kiuchumi na ushirikiano wa kimaendeleo. Juhudi zimekuwa zikifanyika tangu zamani, lakini sasa viongozi wa serikali ya muungano wa vyama vya CDU na CSU na chama cha kiliberali cha FDP, wamekubaliana kwenye mkataba wao wa kuunda serikali, vipi lengo hili linavyonuiwa kufikiwa na katika kipindi gani.

Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, na mwenzake wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel, inatakiwa kuwa ishara ya kwanza - ishara ya ndani ya nchi kwamba wizara hizi mbili zitashirikiana kwa karibu katika siku za usoni.

Ziara ya viongozi hao pia ni ishara kuelekea nje ya Ujerumani, yaani nchi ambazo ni washirika wa Ujerumani. Ishara zote mbili ni muhimu kwani katika vipindi viwili vya bunge vilivyopita, wizara ya mambo ya kigeni na ile ya misaada ya maendeleo zimekuwa zikivutwa nyuma na kuzungukwa na kazi nyingi na vikao vya kuunda mikakati. Ushirikiano kati yao haukifikia kiwango cha kutosha.

Katika nchi washirika, Ujerumani iliwakilishwa na idadi kubwa ya maafisa. Jumbe za Ujerumani zilitumia kiwango kikubwa cha fedha, jambo ambalo lilisababisha gharama kubwa kwa walipakodi wa Ujerumani, wanaogharamia ziara za wajumbe hao. Na kwa nchi washirika, haikuwa kazi rahisi kuwapokea wageni na kusilikiza ushauri tofauti tofauti uliotolewa.

Ikiwa nchini Uganda, Cameroon au Bangladesh kuna wafadhili chini ya darzeni tano, wanaoendeleza sera nzuri ya maendeleo, bila shaka wataanza kuvutana. Hatari ni kubwa kwamba makosa yatatokea, kwa sababu mifumo ya ufisadi imedumishwa. Kwa nini Cameroon inahitaji baraza la mawaziri 60? Kwa nini nchi kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haiwezi kufaulu kuendesha shughuli msingi za serikali na kutoa huduma msingi za kijamii? Hii ni kwa sababu kuna washirika kutoka nje wanaofanya hivyo, ambao kila mmoja anazungumza na sauti yake tofauti na masilahi yao pia ni tofauti.

Katika sera yake ya kigeni Ujerumani inataka kuepukana na hali hiyo katika siku za usoni na imeunda mkakati wake mpya wa Afghanistan, unaozijumulisha pamoja hatua za kiusalama na utoaji wa misaada ya maendeleo. Eneo litakalofuata ni Afrika, ambapo Ujerumani itakuwa na mkakati wa pamoja kujumulisha raslimali za wizara ya mambo ya kigeni na wizara ya misaada ya maendeleo. Kwa njia hii, makosa yaliyofanyika katika miaka iliyopita, yatarekebishwa. Kufungwa kwa taasisi ya Goethe barani Afrika katika miaka ya 1990 kumechangia pakubwa kurudisha nyuma shughuli za Ujerumani barani humo.

Sera ya ushirikiano na Afrika katika serikali mbili za Ujerumani zilizopita, imekuwa tu kama sera ya maendeleo. Katika miaka kumi ya kwanza tangu Ujerumani kuungana, taifa hili limekuwa na sera imara ya nje na nchi za Ulaya Mashariki. Afrika haikupewa kipaumbele, na hilo lilikuwa kosa.

Barani Afrika, Ujerumani inaonekana ikiotea. Nchini Afrika Kusini, ambayo imekuwa mshirika mkubwa wa Ujerumani kwa muda mrefu, sasa China imeipiku Ujerumani na kuisukuma katika nafasi ya pili katika maswala ya biashara. Marekani inataka mwaka 2020 kupata thuluthi moja ya mahitaji yake ya mafuta kutoka barani Afrika.

Hakuna swala lolote la kimataifa linaloweza kutatuliwa bila kuishirikisha Afrika - kuanzia juhudi za Ujerumani kutaka kuwa na kiti cha kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufikia mwisho wa mwaka huu, hadi mkutano wa kilele wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Afrika haiwezi kuwekwa kando!

Na hali ya machafuko kama vile ilivyotokea kaskazini mwa Nigeria au uharamia unaoendelea katika pembe ya Afrika, yote haya ni ishara ya wazi kwamba matatizo ya kisiasa ya Afrika ni kitisho kwa usalama wa Ulaya.

Siasa ya dunia imebadilika sana. Sera kuelekea nchi zinazoendelea na zinazoinukia haraka kiuchumi duniani inatakiwa kujumulisha sera ya nje, uchumi, usalama na maendeleo. Mtazamo huu ni mzuri, lakini bado haujafanyiwa majaribio. Kama mkakati huu unaweza kufaulu kwa upande wa Ujerumani, ni swala la kusubiri na kuona. Na kama utafaulu basi bila shaka sera ya nje ya Ujerumani itaimarika barabara.

Mwandishi: Schaeffer, Ute/ Josephat Charo/ZPR

Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 12.04.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Mti2
 • Tarehe 12.04.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Mti2
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com