Kauli za White House zaendelea kukinzana | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kauli za White House zaendelea kukinzana

Donald Trump amekiri nia ya kitambo ya kumfuta kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika la FBI,James Comey. Na Kaimu Mkurugenzi wa FBI Andrew McCabe amekanusha madai kwamba Comey alikuwa amepoteza imani ya shirika hilo.

Rais wa Marekani Donald Trump amekiri hapo jana kwamba alipanga kumfuta kazi, James Comey, Mkurugenzi wa shirika la upelelezi la Marekani FBI, bila kujali ushauri wa maafisa wa ngazi ya juu wa Wizara ya Sheria. Alisema kwamba alikuwa na nia ya kumfukuza Comey kitambo ila hapajakuwa na muda muafaka wa kufanya hivyo. Kauli hiyo ni kinyuma na taarifa za awali za Ikulu ya Marekani White House. Madai hayo ya Trump yalikuja  baada ya afisa aliyeshika nafasi ya Comey kwa sasa kutoa taarifa zinazokinzana na zile za White House.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani cha NBC, Trump amesema aliwahi kumuuliza Comey kama yupo chini ya uchunguzi na Comey alimhakikishia Trump mara tatu tofauti kuwa hayupo chini ya uchunguzi wa FBI.

"Mimi kwa kweli nilimuuliza, ndio. Nikasema, 'kama itawezekana, je, utanijulisha kama nipo chini ya uchunguzi? Akasema, 'hupo chini ya uchunguzi," amesema Donald Trump.

Trump hakuonyesha wasiwasi wowote kwamba ombi hilo linaweza kutazamwa kama kuingilia katika uchunguzi wa FBI unaohusu madai ya kwamba waendesha kampeni wa kambi yake wakati wa uchaguzi wa 2016, walikuwa na mawasiliano na Urusi iliyoingilia uchaguzi huo kwa lengo la kumpatia ushindi Trump.

Awali Ikulu ya Marekani ilitoa memo kupitia Wizara yake ya Sheria na kutaja kuwa sababu ya kufutwa kazi mkurugenzi wa FBI ni kushindwa kwake kushughulikia uchunguzi wa mwaka jana unaohusu barua pepe za Hillary Clinton. Lakini jana Alhamisi Trump alikiri kwa mara ya kwanza kwamba uchunguzi unaoihusisha Urusi - alioutaja kuwa ni hadithi ya kuzua- ulikuwa ni miongoni mwa sababu zilizompelekea kumfukuza kazi Comey aliyekuwa akiuongoza uchunguzi huo.

Washington Andrew McCabe FBI (Getty Images/AFP/J. Watson)

Andrew McCabe Kaimu Mkurugenzi wa FBI

Kauli za White House zinazobadilika kila siku juu ya kufutwa kazi kwa James Comey zimezua hali ya wasiwasi, huku ikishindwa kua na kauli moja ya kueleweka. Ni hali inayoleta taswira ya rais mwenye hasira.

Trump alimtaja Comey kuwa ni mtu wa kujionyesha na anayependa jukwaa. Maneno hayo ya Trump hata hivyo yalimkasirisha Seneta wa upande wa Democrat Mark Warner. Akizungumza na waandishi habari hapo jana Warner alisema:

"Nimekasirishwa na maoni ya leo ya rais. Hii ni tabia inayoendelea ya kuwavunjia heshima wanawake na wanaume wanaotumika katika jamii yetu ya upelelezi," amesema Mark Warner.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa shirika la upelelezi la Marekani FBI, Andrew McCabe, amesisitiza kwamba shirika hilo litaendelea na uchunguzi dhidi ya Urusi kwa madai ya kuingilia uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2016, kinyume na madai ya Ikulu ya Marekani (White House) kwamba Mkurugenzi aliyefutwa kazi na rais Donald Trump, James Comey alikuwa amepoteza imani ya ofisi hiyo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape,afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com