1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa awasili Goma, DRC

Daniel Gakuba
31 Agosti 2019

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasili Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hii leo, na kuelezea mshikamano na mkoa huo uliokumbwa na machafuko na ugonjwa wa mripuko wa Ebola.

https://p.dw.com/p/3Oo6x
Demokratische Republik Kongo Guterres in Goma
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Gavana wa Kivu Kaskazini Carly Nzanzu baada ya kuwasili mjini GomaPicha: AFP/J. Kannah

Guterres ameanza ziara yake ya siku tatu katika taifa hilo kubwa kieneo, kwenye mji wa Goma ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, ambalo linapambana kukabiliana na Ebolailiyokwisha angamiza maisha ya watu 2000 tangu mwezi Agosti mwaka jana.

Katika kuheshimu utaratibu wa kujilinda dhidi ya maambukizi ya Ebola, Guterres hakushikana mikono na mjumbe wake maalum kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Laila Zerrougui aliyefika uwanjani kumpokea.

Asifu juhudi za kupambana na Ebola

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa  amesema amekuja kuunga mkono juhudi za vikosi vya serikali ya Congo katika mapambano dhidi ya ugaidi ambao ameutaja kuwa kitisho kwa afrika nzima.

Uganda Mpondwe | Medizinisches Personal misst Temperatur - Ebola-Epidemie im Kongo
Juhudi kubwa zinaendelea kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa wa Ebola ambao tayari umeuwa watu zaidi ya 2000 Mashariki mwa DRCPicha: picture-alliance/dpa/AP/R. Kabuubi

Msemaji wake amearifu kuwa Jumapili atafanya ziara kwenye kituo cha kutibu maradhi ya Ebola mjini Beni, na kuzungumza na watu walionusurika ugonjwa huo hatari.

Mji huo wa Beni ulio Kaskazini mwa Goma, umekuwa ukikabiliwa pia na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa waasi wa ADF tangu mwaka 1995, lakini ghasia za waasi hao zimekithiri miaka ya hivi karibuni.

Kundi hilo limewalenga pia maafisa wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Congo, na katika shambulizi baya zaidi dhidi ya maafisa hao lilifanyika Desemba mwaka jana ambapo liliuwa watu 15.

Kitisho cha wanamgambo

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO una jumla ya wanajeshi 16,000. Kwa miaka mingi sasa, makundi ya wanamgambo wenye silaha yapatyo 130 yamekuwa yakishambulia majimbo ya Kivu Kusini na Kaskazini.

Bwana Guterres atakitembelea pia kituo cha kuwarejesha uraiani watu waliokuwa wapiganaji katika makundi hayo kilichopo mjini Goma.

Kwa mujibu wa takwimu za wataalamu wa Chuo Kikuu cha New York pamoja na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, makundi ya wanamgambo yenye silaha yamewateka na kuwauwa raia 1,900 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya mwaka 2017 na 2019.

afpe,