1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katiba mpya yapita Misri

Abdu Said Mtullya23 Desemba 2012

Katiba mpya wa Misri iliyoandikwa na bunge linalodhibitiwa na Waislamu imepitishwa kwa asilimia 64 katika duru ya pili ya kura ya maoni.

https://p.dw.com/p/1789X
Wapiga kura nchini Misri
Wapiga kura nchini Misri,Picha: Reuters

Afisa mmoja wa chama cha Udugu wa kiislamu amefahamisha kuwa katiba mpya ya Misri imepitishwa na wapiga  kura wa nchi hiyo baada ya kufanyika duru ya pili ya kura ya maoni. Afisa huyo ameyakariri matokeo ya kura ambayo siyo rasmi ya chama chake.

Katika duru ya pili ya kupiga kura iliyofanyika hapo jana watu wa Misri waliipitisha katiba mpya kwa asilimia 64. Katika duru ya kwanza asilimia 57 ya washiriki walipiga kura ya ndio. Afisa huyo aliekuwamo katika chumba kilichofuatilia upigaji kura, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa kwa mujibu wa hesabu za chama chake matokeo kamili ya duru ya pili ni asilimia 71 ya kura za ndio.

Rais Mohammed Mursi
Rais Mohammed MursiPicha: AP

Matokeo rasmi kutangazwa Jumatatu

Ameeleza kuwa katika raundi zote mbili kwa jumla, asilimia 63.8 ya wapiga kura waliipitisha katiba mpya. Hesebu hizo pia zimetolewa na Televisheni ya chama cha Udugu wa Kiislamu. Hatahivyo kamati ya kura ya maoni haitayatangaza matokeo kamili hadi hapo kesho baada ya kusikiliza rufani.

Waislamu wanaomuunga mkono Rais Morsi wamesema katiba mpya ni muhimu ili kuweza kuelekea kwenye demokrasia, miaka miwili baada ya kuondolewa kwa utawala wa Mubarak.Watu hao wamesema kwamba katiba hiyo ndio utakuwa  msingi wa kuleta uchumi imara.

Lakini wapinzani wamemlaumu Rais Morsi kwa kulazimisha katiba inayowapendelea Waislamu na kupuuza haki za Wakristo ambao ni asilimia10 ya wananchi wa Misri.Wamesema pia haki za wanawake zimepuuzwa.

Makamu wa Rais ajiuzulu

Wakati huo huo saa chache kabla ya zoezi la kupiga kura kumalizika,Makamu wa Rais wa Misri Bwana Mahmoud Mekky alitangaza kujizulu.Amesema alitaka kuichukua hatua hiyo mwezi uliopita lakini aliamua kuendelea na kazi ili kumsaidia Rais Morsi kuukabili mgogoro uliozuka baada ya Rais huyo kutangaza amri ya kujirundikia mamlaka.

Makamu wa rais aliyejiuzulu Mahmoud Mekky.
Makamu wa rais aliyejiuzulu Mahmoud Mekky.Picha: Reuters

Mekky ambae ni hakimu maarufu amesema hajisikii vizuri katika medani ya siasa, na hapo awali alieleza kuwa hakupewa habari juu ya mpango wa Rais Morsi wa kupora mamlaka. Hata hivyo hatua yake ya kujiuzulu inaambatanishwa na ukweli kwamba chini ya katiba mpya, hautakuwapo wadhifa wa Makamu wa Rais nchini Misri.

Mwandishi:Mtullya Abdu/RTRE
Mhariri:   Ssessanga Iddi Ismail