1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kathrada, mfungwa mwenza wa Mandela afariki

Oumilkheir Hamidou
28 Machi 2017

Mwanaharakati mashuhuri wa Afrika Kusini ,mfungwa mwenza wa Nelson Mandela katika kisiwa cha Robben, Ahmed Kathrada amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87. Kifo chake kimezusha wimbi la rambi rambi kote nchini humo

https://p.dw.com/p/2a6fQ
Ahmed Kathrada
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mbunge huyo wa zamani na mshauri wa karibu sana wa rais Mandela katika uongozi wake wa mhula mmoja kati ya mwaka 1994-1999, Ahmed Kathrada, mwenye asili ya kihindi alikuwa miongoni mwa vigogo wa mwanzo mashuhuri wa chama cha ukombozi wa Afrika Kusini-ANC.

Akijulikana kwa jina la "Uncle Kathy" alijipatia umashuhuri mwishoni mwa miaka ya 80 katika mazungumzo kati ya ANC na serikali ya wazungu wachache, mazungumzo yaliyopelekea kuporomoka enzi za ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid mapema miaka ya 90 na kuitishwa uchaguzi wa kwanza huru mwaka 1994.

Ahmed Kathrada alilazwa hospitali mapema mwezi huu na kufanyiwa opereshini ya kichwa kabla ya hali yake kuzidi kuwa mbaya siku za hivi karibuni.

 

Ahmed Kathrada (kushoto) alipokutana na rais wa zamani wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Roman Herzog na mkewe, mwaka 1998 mjini Berlin
Ahmed Kathrada (kushoto) alipokutana na rais wa zamani wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Roman Herzog na mkewe, mwaka 1998 mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa/A. Zieminski

 Ahmed Kathrada "amefariki kwa amani" katika hospitali ya Donald Gordon

Mmojawapo wa vigogo walio hai wa mapambano ya kihistoria dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid, askofu mkuu wa zamani Desmond Tutu amemsifu Ahmed Kathrada na kumtaja kuwa " mtu mwenye ukarimu,upole na thabiti kupita kiasi."

"Siku moja alimwandikia Mandela na kumwambia haamini kama ni muhimu hivyo kupewa hishma kubwa kubwa" amesema mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel,mwenye umri wa miaka 85.

Serikali inapanga kutoa hishma rasmi kwake na bendera kushushwa nusu mlingoti hadi usiku wa siku ya mazishi-wamesema kwa upande wao maafisa wa ofisi ya rais Jacob Zuma.

"Ni pigo kubwa kwa chama cha ANC, kwa vuguvugu la ukombozi na kwa Afrika Kusini kwa jumla, amesema mkurugenzi wa wakfu wa Ahmed Kathrada, Neeshan Balton.

"Uncle Kathy alikuwa mtu mzuri, binaadam wa kweli na mtu asiyependa makuu,"amesema mwanaharakati mwenzake Derek Hanekom. Alikuwa mwanamapinduzi aliyebobea aliyesabilia maisha yake yote kupigania uhuru nchini mwetu amesema.

Ahmed Kathrada akisikiliza hotuba katika mkutano wa 10 wa kimataifa wa washindi wa tuzo ya amani ya Nobel katika ofisi ya meya wa jiji la Berlin, Novemba 10 mwaka 2009
Ahmed Kathrada akisikiliza hotuba katika mkutano wa 10 wa kimataifa wa washindi wa tuzo ya amani ya Nobel katika ofisi ya meya wa jiji la Berlin, Novemba 10 mwaka 2009Picha: Getty Images/Afp/Leon Neal

Afrika Kusini yamkumbuka Uncle Kathy

Ahmed Kathrada ,mtoto wa wahamiaji wa kihindi-waumini wa dini ya kiislam, alizaliwa Agosti 21 mwaka 1929 katika mkoa uliokuwa wakati ule ukijulikana kama Transvaal Magharibi nchini Afrika Kusini. Alijitoa shuleni akiwa na miaka 17 ili kujiunga na mapambano dhidi ya sheria zinazotenganisha makaazi kwa misingi ya kikabila. Ahmed Kathrada alikamatwa mwaka 1963 pamoja na Nelson Mandela, Walter Sisulu na baadhi ya viongozi wa ANC katika makao makuu yao ya chini kwa chini mjini Johannesburg na kuhukumiwa kwa makaosa ya uharibifu.

Akihukumiwa kifungo cha maisha mwaka uliofuatia, na kupelekwa katika jela ya Roben Island ambako alifunguliwa miaka 26 baadae.

"Alikuwa akinipa moyo tulipokuwa jela, mmwongozo katika maisha yangu ya kisiasa na mhimili katika wakati wa mitihani katika maisha yangu, sasa amekwenda zake" amesema mmojawapo wa wafungwa wenza wa Robben Island, Laloo "Islu" Chiba, mwenye umri wa miaka 86.

Tangu alipostaafu mwaka 1999, Ahmed Kathrada alikuwa akishughulikia wakfu wake aliouunda ili kupambana dhidi ya ukosefu wa usawa.

Aliamua kutokaa tena kimya mwaka mmoja uliopita na kulalamika dhidi ya mkondo unaofuatwa na ANC chini ya uongozi wa rais Jacob Zuma.

Wakaazi wote wa Afrika kusini, wakiwemo pia wana ANC wameelezea masikitiko yao kwa kifo cha mwanaharakati huyo msuluhifu, mpole na mstahamilifu-kama ilivyosema taarifa ya ANC.

 

Mwandishi:Hamidou AFP/Reuters

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman