Kashfa ya malipo ya fedha yazidi kumuandama Fillon | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kashfa ya malipo ya fedha yazidi kumuandama Fillon

Mgombea urais wa chama cha Republican Francois Fillon, huenda akakabiliana na hatua za ziada za kisheria, kwa madai ya kuhakikisha mkewe analipwa maelfu ya fedha  kwa kazi ambayo hakuifanya.

Gazeti la Journal de Dimanche (JDD), limezikariri duru fulani zikisema tukio hilo litaashiria kwamba mwendesha mashtaka ameamua kutoifuta kesi hiyo,  kwa kukosekana ushahidi ikiwa na maana ataendelea  nayo.

Msemaji wa mwendesha mashtaka  alisema hakuna uamuzi uliochukuliwa kwa wakati huu wala hakuna muda maalum uliowekwa, bali uchunguzi unaendelea.

Wakili wa Fillon na mke wake, hakutoa maelezo yoyote kuhusu matamshi hayo. Itakumbukwa Fillon, waziri mkuu wa zamani  katika utawala wa Nicolas Sarkozy, amekiri kwamba mkewe alilipwa maelfu ya euro lakini anashikilia kazi aliyoifanya ilikuwa ni halali.

Frankreich Präsidentschaftswahl - Fillon und Penelope (picture-alliance/abaca/A. Robert)

Mke wa Fillon, Penelope Fillon

Fillon ambaye ameweza hadi sasa kukivuta chama chake upande wake, anapigania kuimarisha kampeni yake na  kusema hatojitoa katika mbio hizo za urais, ikiwa utaanzishwa uchunguzi rasmi dhidi yake.

Utafiti wa maoni ya wapiga kura tangu ilipozuka kashfa hiyo karibu wiki tatu zilizopita, unaonyesha nafasi yake ya ushindi ikizidi kupunguwa.

Wapiga kura wamevunjika moyo kutokana na  ripoti ya gazeti la kila wiki Canard Enchaine, kwamba  mkewe alilipwa euro elfu kadhaa za walipa kodi kwa kazi ambayo huenda hata  hakuifanya, kama mumewe  alivyodai.

Awali ilionekana Fillon  mwenye umri wa miaka 62, alikuwa na  nafasi nzuri ya kushinda, lakini sasa ametupwa katika nafasi ya tatu katika duru ya kwanza ya uchaguzi Aprili 23, matokeo ambayo yatamuacha Marine Le Pen, kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, National Front, katika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Emmanuel Macron, ambaye ni mgombe wa kujitegemea na hivyo wanasiasa hao wawili kuumana katika duru ya pili Mei 7.

Frankreich Le Pen startet Wahlkampf mit Angriffen auf die EU (Reuters/R. Prata)

Marine Le Pen, kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia - National Front

Kwa mujibu wa Journal de  Dimanche, kuna  njia mbili zinazoweza kuchukuliwa na mwendesha mashtaka. Kwanza ni kuiwasilisha kesi hiyo kwa hakimu mchunguzi ambaye jukumu lake ni kuamua kama muhusika au wahusika wachunguzwe rasmi au njia ya pili itakuwa kesi hiyo kupelekwa moja kwa moja katika mahakama ya jinai.

Kama ni njia ya pili itakayotumika, gazeti hilo linasema, mchakato utaanza kwa uchache katika kiipindi cha siku 11.

Mgombea mbadala pindi Fillon atajiondoa

Pindi chama cha Republican kitahitaji kumteuwa mgombea mwingine mpya, siku ya mwisho ya kukusanya saini itakuwa Machi 17.

Kesi ya Fillon na malipo kwa mkewe, imetanuliwa na kuunganishwa na malipo yaliotolewa kwa wanawe wawili. Ofisi ya bunge ya mwanasiasa huyo imepekuliwa na watu wanne kuhojiwa na polisi.

Tayari watu wawili wanaoweza kujaza nafasi yake pindi atajitoa, wanaelekea  hawako  tayari kujaza pengo hilo. Alain Juppe, aliyetokeza  nafasi ya pili nyuma ya Fillon wakati wa kura za mchujo, ameshatamka  kuwa hana  nia ya kuchukua nafasi hiyo na Nicolas Sarkozy  aliyemaliza watatu na kutolewa katika duru ya kwanza ya mchujo, tayari iliamriwa  mnamo Februari 7 afunguliwe mashtaka kutokana  na kukiuka utaratibu wakati alipogombea muhula wa pili 2012 na kushindwa na  Msoshalisti Francois Hollande. Sarkozy  anasisitiza hana kosa lolote na  mawakili wake wamesema watakata rufaa.

Frankreich Macron will verstärkten Kampf gegen Terror (picture alliance/dpa/M. Ollivier)

Mgombe wa kujitegemea Emmanuel Macron

Majina mengine yanayotajwa  na vyombo vya habari vya Ufaransa  kujaza nafasi hiyo pindi Fillon atajitoa, ni pamoja na  Rais wa Baraza la Seneti Gerard Larcher na mawaziri wawili wa zamani, Xavier Bertrand, na  Francois Baroin.

Hata hivyo Baroin alisema mwishoni mwa juma, kwamba suala hilo halipo, kwani chama kina mgombea na wanamuunga mkono.

Utafiti mpya

Utafiti mpya  wa wapiga kura, unaonesha mgombea wa National Front, Marine Le Pen, atapata asili mia 26 ya kura katika duru ya kwanza akifuatwa na Emmanuel Macron asilimia 22 na Fillon asilimia 21. Ikiwa  duru ya pili itakuwa kati ya Le Pen na Macron, Macron atashinda kwa asili mia 63 kwa  37 .

Na pindi itakuwa  ni Le Pen na Fillon, basi Fillon atashinda kwa  asilimia 58 dhidi ya 42.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/rtre

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com