Karzai akataa ombi la Marekani kuhusu mpango wa usalama | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Karzai akataa ombi la Marekani kuhusu mpango wa usalama

Hatima ya majeshi ya Marekani nchini Afghanistan bado iko kwenye mashaka. Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amekataa wito wa Marekani kuitaka nchi hiyo isaini makubaliano ya usalama ifikapo mwishoni mwaka huu.

Karzai anasisitiza kuwa mkataba huo unaweza kutiwa saini tu, badala ya baada ya uchaguzi wa rais wa hapo mwakani. Marekani imesema mara kwa mara kuwa haitasubiri hadi baada ya uchaguzi huo wa Aprili 2014. Kama hapatakuwa na makubaliano, Marekani huenda ikawaondoa wengi wa wanajeshi wake kutoka Afghanistan ifikapo mwishoni mwa mwaka ujao.

Taarifa hiyo inakuja wakati baraza kuu la wazee wa kikabila na wanasiasa nchini Afghanistan, linalofahamika kama Loya Jirga, likiyajadili makubaliano hayo ya usalama baina ya nchi hizo mbili.

Kupitia njia ya simu mapema jana Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry aliwasilisha ujumbe kuwa hali yoyote ya kucheleweshwa haikubaliki, na kwamba mkataba huo unapaswa kusainiwa haraka iwezekanavyo. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema Marekani inahitaji kuhakiisha kuwa patakuwa na ulinzi wa majeshi ya Marekani kama yatasalia nchini Afghanistan baada ya mwaka wa 2014.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai akiuhutumia mkutano wa Baraza Kuu la Afghanistan

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai akiuhutumia mkutano wa Baraza Kuu la Afghanistan

Msemaji wa Karzai hatahivyo amekataa kusema kama rais huyo ameuidhinisha mpango huo au la. Alisema hatua yoyote ya rais itatokana na mapendekezo ya baraza la Loya Jirga. Karzai anasisitiza kuwa usalama mzuri, amani na uchaguzi mzuri ni vitu muhimu vitakavyowezesha kutiwa saini nakala hiyo. Washiriki wengi wa mkutano wa Baraza Kuu la Afghanistan ambao uliingia siku ya pili jana, walionekana kuunga mkono kusainiwa kwa mkataba huo. Lakini waandishi wa habari walikuwa na wakati mgumu kuwasiliana na waliopinga mpango huo, kwa sababu walizuiwa na walinzi.

Afghanistan imekuwa ikilumbana na Marekani kwa zaidi ya mwaka mmoja kuhusiana na muafaka huo wa usalama, tangu ilipotuma majeshi yake nchini humo baada ya wataliban kuondolewa madarakani mwishoni mwa mwaka wa 2001.

Karzai amekuwa na uhusiano dhaifu na Marekani na amekuwa akisitasita kujihusisha na mpango huo wa usalama. Alisema katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha Loya Jirga kuwa “imani yake na Marekani siyo nzuri”. Kwamba “hawaamini nao hawamwaamini”.

Wazee wa kikabila na wanasiasa wanaoshiriki mkutano huo na ambao walichaguliwa na utawala wa Karzai, wanatarajiwa kupiga kura ya kuiunga mkono rasimu hiyo na kumtaka rais auzingatie ushauri wao, na kumwezesha Karzai kujitenga na mchakato huo bila kuukandamiza mpango huo. Baraza hilo Kuu lenye wanachama 2,500 linatarajiwa kutangaza uamuzi wake kesho Jumapili.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com