1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KARSLRUHE : Mbaroni kwa njama ya kuuwa Wamarekani

6 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBSL

Ujerumani imesema hapo jana imewatia mbaroni na watuhumiwa watatu wa itikadi kali za Kiislam kwa kupanga njama ya miripuko mikubwa ya mabomu dhidi ya raia ya Wamarekani na vituo vya Marekani vilioko nchini Ujerumani.

Akizungumza na waandishi wa habari mwendesha mashtaka wa serikali Monika Harms amesema watuhumiwa hao wametaja maeneo waliokusudia kuripuwa ni pamoja na sehemu za disko, vilabu vya pombe na viwanja vya ndege ukiwemo wa Frankfurt ambapo hutembelewa sana na Wamarekani kwa kusheheni mabomu mengi kwenye magari ili kuuwa au kujeruhi watu wengi kadri inavyowezekana.

Naye Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Wolfgang Schäuble akizungumzia tukio hilo anasema raia wake kwa waume wanaweza kuhakikishiwa kwamba maafisa wa usalama wa serikali ya shirikisho na wa taifa wamefanya kazi nzuri na kwamba lazima kila mtu asiathiriwe na tishio hili katika maisha yake ya kila siku na harakati zake za maisha.

Watuhumiwa hao watatu wa kiume Wajerumani wawili na Mturuki mmoja wamerundika zaidi ya kilo 700 za kemikali ya hydrogen peroxide kwenye mapipa.Kemikali kama hiyo ilitumiwa katika mashambulizi ya mwaka 2005 kwenye mfumo wa usafiri wa London na kuuwa watu 56.

Watu hao watatu wanatuhumiwa kuwa wanachama wa kundi la Islamic Jihad Union lenye mafungamano na Al Qaeda.

Watuhumiwa wengine wanane wanachunguzwa kwa uwezekano wa kuwa na dhima katika mipango ya mashambulizi hayo.