Kanzela Merkel ziarani Paris | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.10.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kanzela Merkel ziarani Paris

Mada kuu na Rais Sarkozy ni mkutano wa leo wa Umoja wa Ulaya Brussels.

Angela Merkel

Angela Merkel

Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani, mara tu baada ya kuchaguliwa kwake tena jana kuwa Kanzela wa Ujerumani,aliwasili jana jioni mjini Paris,Ufaransa ,ikiwa ziara yake ya kwanza nchi za nje mara baada ya kuanza awamu ya pili.

Katika karamu ya chakula cha jioni na rais Nicholas Sarkozy wa Ufaransa, Kanzela Maerkel, alielezea nia yake ya kuupanua zaidi usuhuba kati ya Ujerumani na Ufaransa. Shina la mazungumzo yao lakini , ni kuandaa msimamo wao wa pamoja kuhusu mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utaoanza baadae hii leo na kundelea hadi kesho mjini Brussels. Rais Sarkozy, akamualika kanzela Merkel kuhudhuria kumbukumbu ya mwezi ujao-Novemba 11, ya kumalizika vita vya kwanza vya dunia akiwa Kanzela wa kwanza wa Ujerumani kuitikia mualiko huo.

Kanzela Merkel, aliwasili Paris hasa kuzungumza na rais Sarkozy juu ya msimamo wao wa kuchukua katika kikao cha leo na kesho mjini Brussels ,Ubelgiji cha viongozi wa Umoja wa Ulaya.Katika mada zote zitaklazojadiliwa leo na kesho huko Ubelgiji, mapendekezo ya Ujerumani na Ufaransa yatakuwa mamoja-hii ni kwa muujibu wa Rais Sarkozy . Shinani kabisa, ni mkataba wa Lisbon na jinsi ya kupambana na uchafuzi wa mazingira.

Kwa upande wake, kanzela Merkel ametangaza nia yake ya kuimarisha zaidi usuhuba na ushirikiano kati ya Ujerumani na Ufaransa -ushirikiano ambao tayari ni mkubwa .

Kanzela Merkel alisema na ninamnukulu,

" Katika kazi yetu tuliotunga katika serikali ya muungano kwa kipindi cha miaka 4 ijayo , tumeiweka usoni kabisa miradi ya elimu,taftishi za kisayansi na ukuaji uchumi ."

Alisema Bibi merkel jana jioni kabla ya karamu hiyo ya usiku mjini Paris.

"Ni furaha ilioje na heshima kubwa ,Kumkaribisha hapa Bibi Angela Merkel jioni hii."

Alisema rais Sarkozy baada ya makaribisho ya dhati katika Qasri la Elysee aliompa Kanzela wa Ujerumani.

Rais Sarkozy akamualika kanzela Merkel, kuhudhuria kama mgeni wa heshima kumbukumbu za mwezi ujao Novemba 11, mjini Paris katika sanamu la makumbusho ya mwanajeshi asiejulikana hapo "Arc de Triomphe" kukumbuka kumalizika kwa vita vya kwanza vya dunia.

Itakumbukwa kwamba, 1998, aliekuwa rais wa Ufaransa ,Jacques Chirac ,alitoa mualiko kama huo kwa aliekuwa Kanzela wa Ujerumani, Gerhard Schroeder, kwenda Paris kuhudhuria siku hiyo ya kumbukumbu.Bw.Schroeder lakini , tena katika hali ya mabishano alikataa kuitikia mwaliko huo.

Kwa kuupokea mwaliko huo, Bibi Angela merkel atakuwa kwahivyo, Kanzela wa kwanza wa ujerumani kuhudhuria kumbukumbu hizo na kama alivyosema rais Sarkozy,kutoa heshima kubwa kwa Ufaransa.

Siku 2 kabla, Novemba 9, rais wa Ufaransa, anatazamiw nae kuja Berlin, Ujerumani, kuhudhuria kumbukumbu za miaka 20 tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin uliogawa sehemu ya mashariki kutoka ile ya magharibi ya jiji hilo kuu la Ujerumani.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ DPA

Mhariri: Abdul -Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com