1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanzela Merkel akamilisha ziara yake ya ghuba huko Bahrain

27 Mei 2010

Vipi kukuza biashara na Ghuba ?

https://p.dw.com/p/NYRR
Kanzela Merkel na Mfalme wa Saudia.Picha: AP

Katika siku ya mwisho ya ziara yake ya Ghuba la waarabu, Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani, amearifu leo huko Doha, Qatar,kwamba, Ujerumani , inapaswa kuhakikisha kwamba, haikosi kuzitumia fursa za kibiashara katika Ghuba na hasa kutokana na kukua kwa nguvu za uchumi za eneo hilo.

Kanzela Merkel, ameitisha pia kuharakishwa kukamilishwa ufumbuzi wa suluhisho la amani la mgogoro wa Mashariki ya Kati.Kanzela Merkel, alisema hayo akiwa Qatar,katika siku yake ya mwisho ya ziara yake ya siku 4 katika nchi za Ghuba .

"Hatuendi kwa kasi sana" -alisema kanzela Merkel, akirejea manun'guniko yake aliotoa kabla kuwa nchi za Asia, zinajirekebisha bora zaidi kibiashara na nchi za ghuba , kuliko ifanyavyo Ujerumani katika kujenga biashara na eneo hilo. Kushindwa kuchukua hatua kama hizo,alionya Kanzela, kutaifanya Ujerumani isiweze kushindana kibiashara katika Ghuba kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.

Kanzela Merkel, alizungumzia kukamilishwa haraka kwa kwa mazungumzo ya amani ya mzozo wa Mashariki ya Kati na akataja kwamba, serikali katika eneo hilo, hazielewi kwanini maafikiano bado yameshindwa kufikiwa.Bibi Merkel, alitambua pia kwamba, viongozi wa nchi za Ghuba, alikotembelea wameonesha hamu kubwa juu ya vipimo vya thamani ya sarafu ya Euro.

Mradi wa nuklia wa Iran, pia ulizungumzwa wakati wa ziara yake hii ya Ghuba.Alisema karata zote zaweza kuwekwa mezani ikiwa Iran, itakuwa wazi nayo juu ya uwezo ilionao wa kinuklia.Mapema jana, maswali ya uchumi na biashara pia yalituwama mno katika mkutano wake na wanabiashara na wanawake katika baraza la Biashara la Saudi Arabia, mjini Jeddah.

Katika Kikao hicho, waziri wa biashara na viwanda wa saudia ,Abdullah bin Ahmed Zainal, alisema kwamba nchi zao mbili zina shabaha ya kukuza kiwango cha biashara tangu kwa wingi hata kwa thamani ya biashara hiyo.Katika matamshi yake kwenye kikao hicho,aliahidi kupigania biashara huru baina ya Umoja wa Ulaya na nchi za Ghuba la Uarabu.

Mazungumzo yamekuwa yakifanyika tangu miaka 20 sasa,lakini yakikwama kutokana na madai ya Umoja wa Ulaya ya kukuzwa haki za binadamu katika nchi hizo. UU umekuwa na mazungumzo na Baraza la Ushirikiano la nchi za Ghuba linalojumuisha Umoja wa Falme za Kiarabu,Saudi Arabia,Kuweit,Oman,Qatar na Bahrein.

Biashara na Saudi Arabia, imekuwa ikipanda kutoka kima cha dala bilioni 3.2 miaka 6 iliopita hadi dala bilioni 10 mwaka 2008.Wasaudi wamekuwa wakilalamika mara kwa mara, kuwa Ujerumani sheria ni kali kwa watembezi wanaowasili Ujerumani na viza za kibiashara, za utafiti au za matibabu.

Bibi Merkel, akawataka maafisa wa Ujerumani, kuwaachia raia wa Saudia kuingia Ujerumani bila ya vikwazo .Baada ya ziara yake leo huko Qatar, Kanzela Merkel, atatembelea Bahrain,kabla ya kurejea Ujerumani.

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE

Uhariri: Abdul-Rahman