1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Schmidt, leo anatimia umri wa miaka 90

Miraji Othman22 Desemba 2008

Kansela wa zamani Helmut Schmidt atimia umri wa miaka 90 leo

https://p.dw.com/p/GLSp
Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut SchmidtPicha: AP

Kutoka mwaka 1974 hadi 1982, kama kansela, alikamata nyadhifa muhimu kabisa za kisiasa katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Ukansela wake uliangukia katika wakati ambapo Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani lilikabiliana na mitihani mingi ya kisiasa na ya kiuchumi. Na hata miaka thalathini baadae, Helmut Schmidt bado anathaminiwa kama mchambuzi wa mambo ya kisiasa.

Helmut Schmidt alikuwa kansela wa tano wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Hebu isikilize sauti yake pale alipokamata ukansela mwaka 1974:

Insert: 0-Ton Helmut Schmidt...

+Serekali hii ya mseto inakusudia kuendelea na siasa za vyama vya Social Democratic na kiliberali.+

Mei 17, mwaka 1974, Helmut Schmidt alifikia kilele cha harakati zake za kisiasa. Alichaguliwa kuwa kansela watano wa Shirikihsho la Jamhuri ya Ujerumani, kama mrithi wa Willy Brandt aliyejiuzulu kutokana an kashfa iliosababishwa na mtu aliyegundulikana kuwa ni shushushu wa iliokuwa Ujerumani Mashariki, Guillaume. Haiajatarajiwa kwamba angekamata wadhifa huo..

Helmut Schmidt alizaliwa Hamburg Disemba 23, mwaka 1918. Baada ya kumaliza shule ya sekondari ya juu, mwaka 1937 aliingia katika utumishi wa serekali na baadae akaingizwa katika jeshi. Alipokuweko katika medani ya vita huko upande wa Urussi, alijionea mwenyewe vipi vita vilivokuwa, kama alivosema yeye mwenyewe, kinyesi kikubwa. Jambo hilo alisema hatalisahau maisha.

Baada ya vita alijiingiza katika harakati za chama cha Social Democratic, SPD, akawa waziri wa mambo ya ndani wa mkoa wa Hamburg, pale yalipotokea mafuriko makubwa ambayo yaliutishia mji huo na wakaazi wake. Alitumia nguvu zake bila ya kuchelewa kuikabili hatari hiyo. Hivyo akapata umaarufu hata nje ya mipaka ya mji huo.

Insert: O-Ton Sturmflut...

+Ilipendekezwa kwamba watu wabakie katika gorofa za juu, karibu na mapaa ya majumba yao, na sehemu ya mapaa yawe wazi, ili waweze kuokolewa na ngazi zitakazoteremshwa na helikopta. Kutokana na dhoruba za mafuriko helikopta hazikuweza kuwaondoa watu kutoka kwenye madirisha ya majumba yao.+

Katika serekali ya mseto ya vyama vikubwa, chini ya Kansela Kurt Georg Kiesinger, Helmut Schmidt akawa kiongozi wa wabunge wa chamna cha Social Democratic, SPD. Bila ya mikwaruzano na Rainer Barzel, mwenzake wa upande wa vyama vya CDU na CSU, aliandaa mikakati ya ya serekali hiyo ya mseto.

Hatua nyingine ilitokea mwaka 1969, pale alipoteuliwa kuwa waziri wa ulinzi katika serekali ya muungano baina ya vyama vya SPD na kile cha kiliberali cha FDP. Baada ya uchaguzi mpya wa mwaka 1972 akakamata wadhifa wa wizara ya fedha. Uzoefu huo ulimpatia nyenzo baadae za kuwa kansela, hivyo kukamata wahifa muhimu kabisa wa kisiasa katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.

Ukansela wake baina ya mwaka 1974 na 1982 ulikabiliwa na uchumi kwenda chini kote duniani, mzozo wa nchi zinazotoa mafuta kupunguza utoaji wa mafuta na kupanda idadi ya watu wasiokuwa na kazi hapa Ujerumani. Upande wa matatizo ya kiuchumi aliukabili kwa kuanzisha mpango wa kuupiga jeki uchumi. Pia aliianzisha ile fikra ya kufanyika kila mwaka mkutano wa kilele wa dunia juu ya uchumi, hivyo kuweza kukutana wakuu wa nchi muhimu za kiuchumi duniani. Kutokana na jitihada zake, wakuu hao wamekuwa wakikutana kila mwaka.

Helmut Schmidt, lakini, ilibidi audhibiti mtihani mwengine. Ugaidi wa kundi la jeshi Jekundu la mrengo wa shoto ulizidi kuihatarisha dola. Kwa nguvu alikabiliana na maujai yaliokuwa yakifanywa na magaidi. Katika kile cha kile kilichotajwa kuwa ni mapukutiko ya mwaka 1977, mkuu wa jumuiya ya waajiri wa Ujerumani, Hans-Martin Schleyer, alitekwa nyara. Chama cha CDU kililimtaka Helmut Schmidt, kwa muda, aziweke kando baadhi ya kanuni za kidemokrasia ili apambane na ugaidi. Lakini mwanademokrasia huyo maisha alihofia mifano ya kutisha ya enzi za utawala wa Wanazi hapa Ujerumani. Mwenyewe alisema hivi wakati huo:

Insert: O-Ton...

+Mtihani hasa uko kwamba tusikubali usalama wetu ugonganishwe na uhuru. Msingi wetu ni kwamba sisi ni dhidi ya mawimbi ya kutostahamiliana, hali ambayo baadhi ya watu wanataka kuisambaza hapa nchini.+

Kutokana na msimamo huo, dola ililipia gharama kubwa, kwani haijaweza kuyaokoa maisha ya Hans-Martin Schleyer.

Mwanzoni mwa miaka ya thamanini, ilionekana kwamba Chama cha SPD hakiko tena nyuma ya Helmut Schmidt katika majadiliano juu ya uamuzi wa ncha mbili wa Jumuiya ya NATO uliopelekea kuwekwa maroketi mepya hapa Ujerumani Magharibi. Wakati huo huo, kulionekana wazi kuna mkwaruzano katika serekali ya mseto ya vyama vya SPD na FDP. Helmut Schmidt alitaka uitishwe uchaguzi mpya. Lakini baadae wingi wa wabunge wa vyama vya CDU/CSU na FDP walimuengua kuwa kansela. Alisema hivi:

Insert; O-Ton...

+Kuaminika demokrasia maana yake pia kuweko mabadilishano ya serekali. Hivyo silalamiki pale serekali ya vyama vya SPD na FDP inabidi iache dhamana ya kutawala. Kile ambacho bado ninalalamika ni ukosefu wa kuaminika mabadiliko haya na namna ya mabadiliko haya ya serekali yalivofanyika."

Helmut Schmidt aliondoka madarakani, lakini amebakia katika hadahara ya umaa wa Ujerumani. Hivi sasa yeye ni mchapishaji wa gazeti maarufu linalotolewa kila wiki, DIE ZEIT; na bado anaendelea kuthaminiwa kama mchambuzi wa matokeo ya kisiasa.