1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel ziarani Ugiriki

9 Oktoba 2012

Polisi ya Ugiriki imefyetua gesi za kutoa machozi na maguruneti kuwatawanya waandamanaji walipojaribu kuvunja vizuwizi ili kumkaribia kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaeitembelea nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/16MzG
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras mjini AthenPicha: AP

Maelfu ya waandamanaji walivunja amri ya kutoandamana na kukusanyika katika uwanja mkuu wa Syntagma kuelezea hasira zao kwa kansela wa Ujerumani ambae wengi nchini humo wanamtwika jukumu la maisha magumu wanayokumbana nayo wagiriki ili badala yake wapatiwe mikopo ya Umoja wa Ulaya na shirika la fedha la kimataifa iliyopindukia Euro bilioni 200.

Baadhi ya waandamanaji waliwavurumishia polisi mawe,na hata fimbo na kujaribu kuvunja vizuwizi vilivyowekwa kumkinga kansela Angela Merkel na ujumbe wake,waliokuwa wakikutana na waziri mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras katika ofisi yake,umbali wa kilomita mia kadhaa kutoka hapo.

Waandamanaji kadhaa wamekamatwa.

Hii ni ziara ya kwanza ya kansela Angela Merkel nchini Ugiriki tangu mgogoro wa fedha uliporipuka barani Ulaya,miaka mitatu iliyopita.Lengo la ziara yake ni kutoa risala ya mshikamano katika nchi hiyo inayokabwa na ughali wa maisha na kishindo cha kuendelea kuwa mwanachama wa kanda ya sarafu ya Euro.

Griechenland Proteste wegen Angela Merkels Besuch in Athen
Maandamano dhidi ya ziara ya kansela Merkel mjini AthensPicha: AP

Katika mkutano na waandishi habari,mwishoni mwa mazungumzo yake pamoja na waziri mkuu wa Ugiriki,kansela Angela Merkel amewapa moyo wagiriki akisema:"Nnaamini kwamba njia hii,ingawa ni ngumu,lakini ndio itakayoisaidia Ugiriki.Kwasababu ikiwa matatizo hayatapatiwa ufumbuzi hivi sasa,siku zijazo yatazidi kuwa magumu.Ni kwa masilahi yetu ya pamoja tutakaporejesha imani ya walimwengu kwetu sisi barani ulaya na kudhihirisha kwamba sisi katika zoni ya Euro,matatizo tunayafambua kwa pamoja na tunachonga njia ili watoto na wajukuu wetu,miaka inayokuja waweze kuishi katika neema."

Kansela Angela Merkel amesifu maendeleo yaliyoweza kupatikana nchini Ugiriki na kuahidi Ujerumani itaisaidia nchi hiyo katika kuiimarisha mfumo wa afya na shughuli za utawala.

Griechenland Angela Merkel mit Antonis Samaras
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu Antonis SamarasPicha: Reuters

Kwa upande wake waziri mkuu wa Ugiriki Antnis Samaras amemhakikishia kansela Angela Merke nchi yake itaendelea kuheshimu ahadi ilizotoa na inataka kuendelea kuwa mwanachama wa kanda ya Euro licha ya shida zilizoko.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman