1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel ziarani mjini Washington

Oumilkher Hamidou3 Novemba 2009

Kansela Angela Merkel atawahutubia wawakilishi wa mabaraza ya Senet na wawakilishi baadae hii leo

https://p.dw.com/p/KMGS
Rais Obama na kansela Angela MerkelPicha: AP

Katika hotuba yake mbele ya baraza la Congress la Marekani baadae hii leo,mwezi mmoja kabla ya mkutano wa kimataifa mjini Copengahen,kansela Angela Merkel anatarajiwa kuisihi Marekani ipitishe hatua thabiti dhidi ya kuzidi hali ya ujoto ulimwenguni.

Angela Merkel aliyeidhinishwa wiki iliyopita kwa mhula wa pili wa miaka minne,atakutana na rais Barack Obama huko White House kabla ya kuwahutubia wawakilishi wa mabaraza yote mawili ya Congress-baraza la Senet na baraza la wawakilishi.

Fursa hiyo ni ya pekee :Hii ni mara ya pili baada ya Konrad Adenauer mwaka 1957, kwa kansela wa Ujerumani kupewa hishma ya kuhutubia mabaraza yote hayi mawili ya Marekani.

Naibu mwenyekiti wa kundi la SPD bungeni,Gernot Erler anatathmini hotuba ya kansela Angela Merkel katika baraza la Congress kama ifuatavyo:

"Ni hishma kubwa hiyo,ya kwanza tangu Adenauer.Kwa hivyo kila kitu kinategemea hotuba hiyo.Bila ya shaka miongoni mwa mengineyo kuna kumbukumbu za miaka 20 tangu Ujerumani ilipoungana na mchango wa maana uliotolewa na Marekani.Kuna matatizo ya kimataifa ambayo tunataraji atayazungumza wakati wa mkutano wake pamoja na rais Barack Obama,na miongoni mwa mada katika hotuba yake ,kwa mfano maandalizi ya mkutano wa kilele wa umoja wa mataifa kuhusu hali ya hewa mjini Copenhagen."

Merkel auf dem G-20 Gipfel in Pittsburgh
Kansela Angela MerkelPicha: DPA

Kabla ya kwenda Washington,kansela Angela Merkel alisema katika risala yake kupitia mtandao wa internet kwamba mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa ndio mada mojawapo kuu itakayogubika ziara yake nchini Marekani.

"Ni jukumu la kimataifa ambalo hatuwezi kuliakhirisha"-amesisitiza.

Hotuba ya kansela Angela Merkel ni fursa kwa hivyo ya kuwasemesha moja kwa moja wawakilishi wa Marekani na kuwakumbusha kwamba ulimwengu umekodoa macho Washington,linapohusika suala la kuzidi hali ya ujoto duniani.

Kwa mujibu wa viongozi wa serikali,hotuba ya kansela Angela Merkel itadumu dakika 30 na ataitoa kwa lugha ya kijerumani.

Mbali na mada kuhusu hali ya hewa,kansela Angela Merkel atazungumzia pia umuhimu wa uhusiano kati ya Marekani na Ujerumani,na mchango wa Marekani katika kuporomoka ukuta wa Berlin .Kansela Angela Merkel atazungumzia pia suala la vita nchini Afghanistan na mradi wa kinuklea wa Iran-mada mbili ambazo pia zitagubika mazungumzo yake pamoja na rais Barack Obama.

Mwandishi :Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Abdul-Rahman