1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel ziarani barani Afrika

Oummilkheir5 Oktoba 2007

Kansela Angela Merkel azungumza na rais Thabo Mbeki

https://p.dw.com/p/C786
Kansela Merkel,,bwana Alpha Omar Konare na John Kufour wakiwakumbuka wanajeshi 10 wa Afrika waliouliwa Darfour
Kansela Merkel,,bwana Alpha Omar Konare na John Kufour wakiwakumbuka wanajeshi 10 wa Afrika waliouliwa DarfourPicha: AP

Kansela Angela Merkel anaendelea na ziara yake barani Afrika. Kiongozi huyo wa serikali kuu ya Ujerumani amewasili Afrika kusini jana usiku,kituo cha pili cha ziara hii itakayomfikisha pia Liberia.Lengo la ziara ni kuhimiza utawala bora ,kuheshimiwa haki za binaadam pamoja na kuimarishwa uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na bara la Afrika.

Kansela Angela Merkel amekaribishwa kwa heshima za kijeshi na mwenyeji wake rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini mjini Pretoria.Duru za kuaminika zinasema miongoni mwa mada mazungumzoni ni pamoja na hali katika nchi jirani ya Zimbabwe ambako rais Robert Mugabe analaumiwa kwa kuitumbukiza nchi yake katika hali ya kufilisika.

Leo jioni kansela Angela Merkel aliyefuatana na ujumbe wa wanauchumi,na meneja wa timu ya taifa ya kabumbu ya Ujerumani Oliver Bierhoff,atakwenda Johanneburg,kuzuru kiwanja cha michezo “mtaa wa kabumbu” kinachojengwa kwaajili ya fainali za kombe la dunia mwaka 2010 .Amepangiwa pia kuzungumza na rais mstaafu wa Afrika kusini Nelson Mandela kesho kabla ya kwenda Cape Town kwa mazungumzo pamoja na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani,Hellen Zille .

Uhusiano kati ya nchi hizi mbili ni mzuri .Afrika kusini ni mshirika mmojawapo muhimu wa kiuchumi kwa Ujerumani barani Afrika.Biashara ya nchi hizi mbili imeongezeka mara nne tangu kumalizika utawala wa ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid.Kwa kipindi cha mwaka jana Ujerumani imesafirisha bidhaa zenye thamani ya yuro bilioni tano nukta sabaa.Thamani ya bidhaa za kutoka Afrika kusini zilizoingia Ujerumani inakadiriwa kufikia nusu tuu ya kiwango hicho cha fedha.

Licha ya mizozo ya Darfour,Zimbabwe na Somalia,bara la Afrika linainuka kiuchumi.Ukuaji wa kiuchumi wa wastani unafikia asili mia tano na katika baadhi ya nchi ukuaji wa kiuchumi unagonga asili mia nane.

Mara nyingi lakini hali hiyo ya kutia moyo haipigiwi upatu na vyombo vya habari vya magharibi.

Katika mahojiano pamoja na maripota kabla ya mazungumzo yake pamoja na kansela Angela Merkel,rais Thabo Mbeki alisema:

“Nadhani ni muhimu kuzungumzia ukweli halisi.Na ukweli halisi ni kwamba kuna maendweleo mengi ya kutia moyo barani Afrika.”

Kabla ya Afrika kusini, kansela Angela Merkel alikua Ethiopia ambako alizungumza na waziri mkuu Meles zenawi na kuhutubia mbele ya wawakilishi wa Umoja wa Afrika.Kansela Angela Merkel aliitolea mwito jumuia ya kimataifa itathmini upya uhusiano wake kuelekea bara la Afrika na kuhimiza utawala bora pamoja na kuheshimiwa haki za binaadam .

Kituo cha mwisho cha ziara ya kansela Angela Merkel ni Monrovia ambako jumapili ijayo anatazamiwa kuonana na rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia.