1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel kukutana na wakuu wa majimbo kuhusu COVID-19

Daniel Gakuba
1 Februari 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anakutana leo na wakuu wa majimbo kujadili mpango wa chanjo nchini humo. Umoja wa Ulaya umepiga hatua katika kuzishinikiza kampuni za kutengeneza chanjo kuupatia dozi zaidi.

https://p.dw.com/p/3ofAI
Berlin I Angela Merkel verkündet Verlängerung des Lockdowns
Kansela Merkel (katikati) akielekea kwenye mkutano na waandishiPicha: Michel Kappeler/REUTERS

Mkutano huo wa video kati ya Kansela Merkel na wakuu wa majimbo utahudhuriwa pia na wawakilishi wa watengenezaji wa chanjo na Halmashauri ya Ulaya. Wakuu wa majimbo kadhaa ya shirikisho wametaka ufafanuzi juu ya viwango vya dozi za chanjo na muda wa kuwasilishwa dozi hizo, kufuatia mkanganyiko uliojitokeza katika zoezi hilo.

Soma zaidi:  Umoja wa Ulaya watangaza taratibu kali za kudhibiti mauzo ya chanjo dhidi ya corona

Waziri wa Afya Jens Spahn alijaribu kupunguza matarajio kabla ya mkutano huo, akiliambia jarida la kila siku la Bild kwamba mkutano huu pekee hauwezi kufanikisha uzalishaji wa chanjo zaidi. Spahn alisema upatikanaji wa dozi za kutosha za chanjo ndio changamoto kubwa kwa wakati huu.

Mafanikio yahitaji mpango wa kitaifa

Meya wa mji mkuu, Berlin Michael Müller aliamuandikia barua kansela Merkel, akisema ikiwa Ujerumani inataka kufanikiwa kuwachanja watu wake ifikapo mwezi Septemba, mpango wa kitaifa unahitajika.

Deutschland Impfzentrum Brandenburg  Coronavirus
Shughuli ya kutoa chanjo ya corona Ujerumani imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa doziPicha: imago images/Jochen Eckel

Taasisi ya Robert Koch inayodhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani wakati huo huo imeripoti maambukizo mapya 5,608 na vifo 175 katika masaa 24 yaliyopita.

Soma zaidi: WHO yaanza kuchunguza chimbuko la corona, China

Kwingineko Ulaya, kampuni ya AstraZeneca imekubali kusambaza dozi milioni 9 za chanjo yake kwa Umoja wa Ulaya mnamo robo hii ya kwanza ya mwaka 2021, hii ikiwa ni kwa mujibu wa umoja huo.

Ahadi zaidi za chanjo

Ahadi  mpya ya  dozi milioni 40 kufikia mwisho wa Machi bado ni nusu tu ya ile ambayo kampuni hiyo ilikuwa imeiltoa hapo awali kabla ya kutangaza upungufu juu ya shida za uzalishaji.

Portugal | Coronavirus
Watu 175 wamekufa kutokana na COVID-19 katika muda wa saa 24 zilizopitaPicha: Pedro Nunes/REUTERS

Kampuni nyingine, BioNtech-Pfizer amesema itaupa Umoja wa Ulaya dozi milioni 75 za chanjo ya corona  katika robo ya pili ya mwaka 2021.

Huko Mashariki ya Kati, Israeli hapo jana ilirefusha muda wa vikwazo vya kitaifa vya kuzuia maambukizi ya COVID-19, kutokana na hofu ya kuenea kwa aina mpya ya virusi vya corona.

Soma zaidi:Maambukizi ya Corona yapindukia milioni 100

Na nchini Marekani, kundi la maseneta 10 wa chama cha Republican walipendekeza mpango wao kuhusu msaada wa kupambana na athari za janga la corona.

Katika barua waliyomuandikia  Rais Joe Biden, Warepublican hao wanataka fuko kwa ajili ya msaada huo lipatiwa dola bilioni 600 tu, badala ya dola trilioni 1.9 inayopendekezwa na rais huyo.

 

Chanzo: https://p.dw.com/p/3oeVZ