Kansela Merkel aweza kushinda, lakini akampoteza Schäuble | Uchaguzi wa Ujerumani 2017 | DW | 21.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Ujerumani Yaamua

Kansela Merkel aweza kushinda, lakini akampoteza Schäuble

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anapigiwa upatu kushinda uchaguzi ujao wa tarehe 24 Septemba, lakini huenda akampoteza waziri wake wa fedha Wolfgang Schäuble, kwa sababu vyama vingine muhimu vinaitaka wizara ya fedha.

Deutschland Kabinettssitzung Berlin | Finanzminister Wofgang Schäuble, CDU (Getty Images/A. Berry)

Wolfgang Schäuble, wizara yake ya fedha inakodolewa macho na vyama vyote

Waziri Wolfgang Schäuble amekuwa mhimili wa nidhamu ya kifedha, na mtu muhimu kabisa katika serikali ya Kansela Angela Merkel. Ingawa wengi wanaamini kuwa ushindi wa Bi Merkel katika uchaguzi wa Septemba 24 ni kitu kisichotiliwa shaka, kurejea kwa Schäuble katika wizara ya fedha hakutakuwa rahisi.

Utafiti wa wapiga kura unaashiria kuwa chama cha Christian Democratic Union- CDU cha Angela Merkel kitarazimika kutafuta washirika katika kuunda serikali. Chama cha Social Dempcratic, SPD ambacho ni mshirika mdogo katika serikali ya sasa, kimeweka kukabidhiwa wizara ya fedha kuwa sharti la kurejea tena katika ushirika huo. Hiyo ni kwa sababu kwa maoni ya chama hicho, Schäuble anakwenda mbali sana katika sera zake za utengamano wa kifedha.

Wapinzani wa Kansela Merkel wanaamini kwamba kung'ang'ania kwa waziri Wolfgang Schäuble, kwamba Ujerumani na nchi nyingine zilizo katika umoja wa sarafu ya euro, lazima ziheshimu sheria za kibajeti, kunaweza kumnyima rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron uhuru wa kuufufua uchumi wa nchi yake.

Kuikwamua Ufaransa kiuchumi

Deutschland | ARD-Sommerinterview mit Angela Merkel (picture-alliance/dpa/M. Gambarini)

Kansela Angela Merkel, ushindi wake katika uchaguzi ujao hautiliwi shaka

Ujerumani ina ziada ya bejeti itokanayo na kodi, lakini Ufaransa inajikuta katika hali ya kubanwa, na chama cha SPD kinahofu kuwa ikiwa Macron hatafanikiwa kuinua uchumi, hali hiyo itamnufaisha mwanasiasa wa mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen.

Kuna taarifa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye anatoka chama cha SPD, alimtaka Kansela Merkel kuchagua moja kati ya Ufaransa ambayo kidogo inapindisha sheria za kibajeti, au miaka mitano ya urais wa Marine le Pen. Gabriel alisisitiza kuwa lazima Ujerumani ibadilishe msimamo wake.

Kulegeza msimamo kwa waziri Wolfgang Schäuble hakutawafurahisha wajerumani wengi. Katika jimbo lake la Baden-Wuerttemberg, Schäuble anaheshimiwa sana, kwa sababu katika jimbo hilo, bidii kazini pamoja na kuweka akiba ni mtindo wa maisha. Maoni ya Schäuble ni kwamba serikali zinapaswa kujilimbikizia madeni, ili kuwaachia fedha za matumizi watunga sera wa siku za usoni.

Schäuble aashiria azma ya kuendelea na siasa

Frankreich Schulz trifft Macron (picture alliance/dpa/POOL Stern/M. Weiss)

Martin Schilz wa SPD (kulia), chama chake kinataka sera zinazomrahisishia kazi Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (kushoto).

Kwa Schäuble ambaye hutembea katika kiti cha gurudumu tangu alipopigwa risasi na mtu mwenye akili punguani siku chache baada ya Ujerumani kuungana tena mwaka 1990, kazi ni maisha, na anaashiria yuko tayari kuendelea na siasa.

Lakini kazi ya kuunda serikali ya mseti haitakuwa rahisi kwa Kansela Merkel. Vyama viwili ambavyo huenda vikawa chaguo lake wakati atakapokuwa akitafuta washirika baada ya uchaguzi, SPD na FDP chenye sera rafiki kwa biashara, vyote vinaikodolea macho wizara ya fedha.

Sigmar Gabriel amesema katika mkutano mmoja na waandishi wa habari, kwamba chama chake, SPD hakitafanya tena makosa kama ya miaka 4 iliyopita. Mwanachama mwingine muhimu wa chama hicho, amesema ikiwa watalazimika tena kuingia katika serikali ya mseto na CDU, wizara ya fedha itakuwa kigezo muhimu. Hata wanasiasa wa ngazi ya juu wa chama cha CDU wanafahamu wazi kuwa itakuwa vigumu kuinyima SPD wizara ya fedha.

Ni suala la kusubiri na kuona ikiwa kansela Merkel atakuwa tayari kumpoteza Schäuble. Ikiwa hilo litatokea, atakuwa amepata pigo kubwa katika azma yake ya kuimarisha ushirikiano katika Umoja wa Ulaya baada ya Uingereza kuondoka, au hata angalau kuboresha ushirikiano katika kanda inayotumia sarafu ya euro.

Mwandishi: Daniel Gakuba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com