Kansela Merkel atimiza ahadi zake za Copenhagen? | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.03.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kansela Merkel atimiza ahadi zake za Copenhagen?

Watetezi wa mazingira wanadai amevunja ahadi.

Angela Merkel

Angela Merkel

Je, Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani, anatimiza ahadi anazotoa kwa nchi changa katika vita vya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa ?

Yadhihirika, hatimizi ahadi zake, kwani serikali ya Ujerumani imetenga katika bajeti yake ya sasa Euro milioni 70 tu kuchangia juhudi za kimataifa za kuzuwia uchafuzi wa hali ya hewa. Kilichoahidiwa lakini, kilikuwa kima mara 6 kikubwa zaidi kuliko hicho.

Ilikuwa iwe ishara ya kutia moyo ambayo Kansela Angela Merkel aliyekuwa waziri wa mazingira kati ya 1994 na 1998 alioitoa binafsi mjini Copenhagen kwa walimwengu. Kima cha Euro milioni 420 aliahidi kutoa kwa nchi changa hatua kwa hatua kila mwaka hadi 2012 ili zipambane na athari za uchafuzi wa hali ya hewa. Hizo ni fedha ambazo nchi masikini zingezihitaji sana. Kwani watabiri wa hali ya hewa wameshaagua kuwa nchi masikini kabisa ndizo hasa zitakazoathiriwa na ukame na mafuriko.

Hata kabla ya mkutano huo wa kilele huko Copenhagen ulioitishwa na Umoja wa Mataifa ,mashirika yanayopambana na uchafuzi wa mazingira yalionya kwamba hata fedha zaidi zingehitajika na sio zile zilizomo katika bajeti. Ni hali hii hasa, ndio iliyoibuka sasa, wanadai wajumbe wa chama cha Kijani cha walinzi wa mazingira na wa chama cha kijamaa cha SPD. Fedha zilizotolewa ni Euro milioni 70 tu.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Ulrich Wilhelm, anakanusha kuwa Ujerumani haitimizi ahadi ilizotoa za kuzuwia uchafuzi wa hali ya hewa. Anasema, "Kutokana na maarifa yangu na inavyojua serikali ya Ujerumani, ahadi za mchango wa fedha ilizotoa serikali ya Ujerumani, wakati wa mkutano wa kilele juu ya mabadiliko ya hali ya hewa uliofanyika Copenhagen, zimetimizwa. Ujerumani katika mwaka huu wa 2010 hadi 2012 itachangia kima cha wastani cha Euro milioni 420 kugharimia miradi ya kuzuwia uchafuzi wa hali ya hewa katika nchi changa."

Kutoka kima cha Euro milioni 420 ni Euro milioni 70 tu zinazotolewa ambazo nusu zinatoka kwenye mfuko wa wizara ya mazingira na ya misaada ya maendeleo. Nusu nyengine iliyobaki, inatoka kwenye mradi wa kulinda mbuga na kwenye mfuko wa biashara ya kuuza viwango vya gesi zinazochafua mazingira. Miradi yote hiyo miwili ilikwishapangwa 2008. Hivyo ni kusema huo ni muda mrefu hata kabla ya mkutano wa kilele wa Copenhagen, 2009.

Msemaji wa maswali ya bajeti wa chama cha kijani cha walinzi wa mazingira Alexander Bonde anasema, "Tunahisi ni aibu kumuona Kansela akiahidii fedha huko Copenhagen, ambazo hazimo katika bajeti yake ya sasa. Hii ni kuvunja kabisa ahadi kwa nchi zinazoinukia kiuchumi na nchi changa, ambazo zilikuwa tayari kushirikiana na nchi za viwanda katika juhudi za kuzuwia uchafuzi wa hali ya hewa ulimwenguni. Yasikitisha kuona sasa, ahadi alizotoa Kansela hazina thamani."

Kwa jicho la bajeti iliopangwa kwa mwaka huu 2010 asema katibu wa Shirika la ulinzi wa mazingira "GERMANWATCH", Christoph Bals, sera za mazingira za serikali ya sasa ya muungano ya Ujerumani ya vyama vya CDU/CSU na FDP, haiaminiki. Ni kima kidogo tu cha fedha, kilichotolewa na serikali hiyo. "Na hii sio ishara iliotarajiwa kwa vita vya kupambana na uchafuzi wa mazingira ulimwenguni," alisema Bals.

Mwandishi: Füstenau,Marcel (DW Berlin)

Mtayarishi: Ramadhan Ali

Uhariri: A.Mtulya

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com