1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel alaani shambulio la Hanau

Amina Mjahid
20 Februari 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amelaani kile alichokiita sumu ya ubaguzi baada ya mshambuliaji anayeshukiwa kuwa na imani za itikadi kali kuwauwa watu 9 katika baa moja ya shisha na mgahawa mjini Hanau, Ujerumani

https://p.dw.com/p/3Y4Nz
Deutschland Berlin | Statement Angela Merkel, Bundeskanzlerin | Hanau Schießerei
Picha: Getty Images/S. Gallup

"Ubaguzi ni sumu, chuki ni sumu na sumu hii ipo katika jamii zetu na ndio inayopaswa kulaumiwa kwa uhalifu mwingi; " alisema Kansela Merkel akiwa mjini Berlin, akilaani tukio hilo la mwanamume mmoja kufayatua risasi na kuwauwa watu tisa huku wengine wakijeruhiwa katika mji wa Hanau nchini Ujerumani.

Merkel ameongeza kuwa leo ni siku ya huzuni nchini kote.

"Leo ni siku ya huzuni mkubwa nchini mwetu, uchungu mkubwa kuhusiana na vifo vya raia wetu wengi unasikika na watu wa Hanau, kwangu mimi  na kote nchini Ujerumani. Hatumbagui raia yeyote kufuatia nakotoka au dini, tunapinga hatua zozote za kuwagawanya wajerumani kwa nguvu zetu zote," alisema Merkel

Kwa upande wake rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amemuunga mkono Kansela Merkel kwa kulaani matendo ya kigaidi mjini Hanau, huku akisema anasimama na wale wote wanaohisi kitisho cha ubaguzi na kwamba hawapo peke yao.

Rais wa Halmashauri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen, pia amepaza sauti yake juu ya hili na kuelezea kushitushwa na tukio hilo huku rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiandika katika mtandao wake wa kijamii wa twitter kwamba anamuunga mkono Merkel katika kupigania maadili na kulindwa kwa demokrasia.

Shambulio limechochewa na chuki dhidi ya wageni

Deutschland Hanau | Schießerei & Tote, Angriff auf Shisha-Bars: Sicherkräfte vor Eingang einer der Shisha Bars
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Probst

Mshukiwa wa shambulio hilo aliye na miaka 43 allietambuliwa kama Tobias R alipatikana amefariki nyumbani kwake baada ya masaa mengi ya kumtafuta. Mwili wa mamake aliyekuwa na umri wa miaka 72, pia ulipatikana nyumbani humo katika kile kinachotajwa kuwa tukio la kujitoa uhai.

Kulingana na waendesha mashtaka wanaochunguza masuala ya kigaidi wanaoishughulikia kesi hiyo, wameona suala la chuki dhidi ya wageni likichochea tukio hilo lililotokea hapo jana, ambapo tayari kidole cha lawama kimenyooshewa wafuasi wa itikadi kali.

Kwa upande wake waziri wa ndani wa jimbo la Hesse Peter Beuth, amesema mshukiwa ameacha manifesto na vidio katika mtandao wa kijamii inayoonesha nia yake ya shambulizi la kigaidi  lililochochewa na chuki dhidi ya wageni.

Aidha taasisi ya wakurdi nchini Ujerumani katika taarifa yake imesema miongoni mwa waliouwawa katika tukio hili ni watu wa asili ya kikurdi huku ikisema imekasirishwa na serikali ya Ujerumani kutofanya juhudi za kutosha kupambana na ubaguzi unokuwa kwa kasi nchini humo.

Chanzo: AFP/dpa