1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel amemaliza ziara yake katika Bara la Asia

31 Agosti 2007

Kansela Angela Merkel, akiwa amemaliza ziara yake huko Uchina na Japan, amezitaka nchi zenye chumi zenye kuibuka ziweke malengo wazi ya kupunguza moshi mchafu hewani ili kuzuwia ujoto duniani. Pia amesema anataka kupendekeza kwa nchi zinazoendelea suluhu ya mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa, lakini alionya kwamba mashauriano yatakuwa magumu.

https://p.dw.com/p/CH8d
Kansela Bibi Angela Merkel wa Ujerumani akizungumza na Mfalme Akihito wa Japan, katikati akiwa ni mkalimani
Kansela Bibi Angela Merkel wa Ujerumani akizungumza na Mfalme Akihito wa Japan, katikati akiwa ni mkalimaniPicha: AP

Kwa mara nyingine tena katika ziara ya nchi za kigeni, Kansela wa Kijerumani ameionesha ile staili yake. Angela Merkel anathamini sana kuambiana ukweli, hazunguki zunguki katika maneno, huliita pauro kwa jina lake, yaani pauro. Mbele ya wenyeji wake huko Peking, alizungumzia wazi wazi juu ya haki kwa watu kujielezea kile wanaochofikiria, na pia umuhimu wa kulindwa haki za binadamu. Malalamiko kama hayo aliyoyatoa hayatakiwi, na hayaendi sambamba na ule upole na murua za watu wa Asia.

Wakitilia maanani maslahi ya kiuchumi, watangulizi wa Bibi Merkel, kansela wa Chama cha Social Democratic, Gerhard Schroader, na yule wa Chama cha Christian Democratic, Helmut Kohl, walijizuwia kuzizungumzia hadharani mada hizo. Huenda hata hawajazizungumzia kabisa.

Na hata katika mada, kama ya ulinzi wa mazuingira, kansela Merkel hajafunga mdomo wake. Wachina aliozungumza nao, angalau hawajafurahishwa kuzungumzia juu ya mada hiyo. Kwani Uchina katika miongo ya karibuni imeliweka chini suala la mazingira katika orodha, ukilinganisha na maslahi yake ya kiuchumi.

Maneno wazi yanafurahisha, lakini isitarajiwe kabisa kwamba viongozi wa Uchina mara baada ya Bibi Merkel kuchomoza huko Beijing wataielekeza dira yao upande mwengine katika masuala ya haki za raia na hifadhi ya mazingira.

Lakini itambuliwe kwamba Bibi Angela Merkel ameamua kwamba suala la hatari ya kubadilika hali ya hewa duniani libakie kuwa juu kabisa katika ajenda ya masuala ya kisiasa. Pia alipofanya ziara katika mji wa Kyoto, huko Japan, kama ishara, hajatafuna maneno yake. Katika mji huo, miaka kumi iliopita, akiwa waziri wa mazingira wqa Ujerumani, aliitia saini ile Itifaki ya Kyoto ambayo inataka kupunguzwe hewa chafu duniani kote. Mahala hapo palikuwa ni jukwaa zuri la kuutangaza mpango wake wa kulinda hali ya hewa ambao pia utaziingiza nchi zinazoinukia, Uchina na India. Kwa umbali gani nchi mbili hizo zitaufuata mpango huo ni jambo la kungoja na kuona.

Risala hiyo inaweza pia ikatoa matunda hapa Ujerumani. Angela Merkel sasa ameikumbatia mada hiyo, tena kwa hisia nzuri, ambayo hadi sasa imekuwa ikichukuliwa na chama cha upinzani cha Kijani kama ni yao. Kutokana na habari za kutisha zinazotangazwa kila siku juu ya mabalaa ya hali ya hewa, mafuriko na vipindi vya ujoto mkubwa, mada hii ya hali ya hewa itawagusa pia watu katika uchaguzi mkuu ujao wa bunge.

Katika ziara yake ya Asia, Angela Merkel amejionesha kama ni mwanasiasa wa kitaifa na wa kimataifa, akiwaelezea watu kwamba suala la ulinzi wa hali ya hewa duniani ni mtihani mkubwa kabisa wa karne ya 21, na hivyo linataka lipatiwe suluhisho.. Bila ya shaka, vitendo vinatakiwa vifuate, kama kawaida, pale wanasiasa wanapoahidi. Na hasa katika suala la ulinzi wa hali ya hewa, matokeo hayawezi kuonekana fumba na kufumbua.

Angela Merkel hivi sasa anaweza kusema amefanikiwa. Mtangulizi wake, aliyeshindwa, Gerhard Schroader, siku ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi, alimuelezea kwa hasira hasimu wake huyo, tena mbele ya kamera kwamba hataweza kuuendesha uchumi. Gerhard Schroader, aliyepewa jina la Kansela wa Magari kutokana na kujihusisha na kuvipendelea viwanda vya magari, alikosea. Bibi Markel anaweza kuuongoza uchumi.