Kanisa Katoliki limetoa mtazamo mpya wa kisheria kukabiliana na matukio ya udhalilishaji wa kingono dhidi ya watoto. | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.07.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kanisa Katoliki limetoa mtazamo mpya wa kisheria kukabiliana na matukio ya udhalilishaji wa kingono dhidi ya watoto.

Waathirika wakosoa sheria hiyo.

Papa Benedict wa 16,ambaye wakati huo akijulikana kama Kadinali Joseph Ratzinger,akiwa katika shughuli za ibada mwaka 2005.

Papa Benedict wa 16,ambaye wakati huo akijulikana kama Kadinali Joseph Ratzinger,akiwa katika shughuli za ibada mwaka 2005.

Kanisa Katoliki duniani,limetoa mtazamo mpya wa kisheria dhidi ya matukio ya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya watoto kwa mapadri,ikiwa ni jitihada za mwisho kujaribu kulitatua sakata lililolikumba kanisa hilo katika siku za hivi karibuni.

Lakini licha ya jitihada hizo za kanisa,waathiriwa wa matukio ya udhalilishaji huo uliofanywa na mapdri,wameukosoa mpango huo,na kuuelezea kuwa una kasoro,na hauna mabadiliko makubwa.

Msemaji wa Vatican Federico Lombardi ameeleza kuwa sheria hizo mpya za kukabiliana na tatizo la mfadhaiko wa kuwatamani kingono watoto wadogo, linalofanywa na baadhi ya mapadri,na kueleza kuwa hiyo ni ishara ya wazi kuwa kanisa sasa limeanza kuchukuwa hatua dhidi ya malalamiko kama hayo.

Lombardi,ameeleza kuwa kanisa litaendelea na uchunguzi wa ndani kwa lengo la kulinda heshima ya kila mmoja aliyehusishwa na matukio hayo,kauli ambayo imepingwa vikali na asasi ya waathirika wa matukio ya udhalilishwaji huo ya SNAP,iliyoeleza kuwa imefadhaishwa mno na sheria hiyo.

Taarifa za ndani zimeeleza kuwa kitabu hicho cha mafundisho ya sheria hizo cha mwongozo wa kanisa,kiliandaliwa na kiongozi wa kanisa Katoliki, Papa Benedikt wa 16,ambaye wakati huo alikuwa ni Kadinali Ratzinger,kiongozi wa kiroho wa waumini wa kanisa hilo.

Hata hivyo,Mkurugenzi wa asasi ya SNAP,David Clohessy ameikosoa sheria hiyo kwa kueleza kuwa bado inawalinda makasisi wasio waaminifu,na kueleza kwamba matukio ya udhalilishaji watoto kingono,yanapaswa kuripotiwa kwa polisi,na kulitaka kanisa kuweka sera hiyo na kuishurutisha kufanya kazi.

Mwandishi habari wa Vatican Andrea Tornielli kwa upande wake ameeleza kuwa amepongeza sheria hiyo ya Kanisa na kueleza kuwa imezidisha ugumu wakati ambapo sheria zingine bado zinafuatwa,hivyo ameeleza kuwa hazitakuwa sheria za ndani tu,bali pia zinaweza kuwa ni kanuni na utaratibu mzuri ambao unapaswa kufuatwa.

Hata hivyo,kauli hiyo imepingwa na asasi ya SNAP,ambayo imeeleza kuwa matukio ya udhalilishaji watoto kingono hakutokani na suala la kanuni na utaratibu wa kanisa,bali kunachangiwa na suala la kuwepo usiri mkubwa unaofanywa na baadhi ya viongozi wa kanisa, na kueleza kuwa matukio mabaya hayapaswi kuainishwa kwenye kanuni tu,bali yanapaswa kukomeshwa kabisa.

Roberto Mirabile,kiongozi wa kundi la kiitalia la kusaidia walioathirika liitwalo ``La Caramella Buona``, ameeleza kuwa licha ya jitihada kubwa za Papa Benedict wa 16 kutafuta njia ya kulitanzua tatizo hilo,lakini amesikitishwa na kutofuatwa na Makadinali wengine,ili kujuwa ni kesi ngapi ambazo wao wamezipokea zinazohusiana na udhalilishaji huo wa kingono.

Hivyo,amefafanuwa kwamba hadi itakapofikia hatua hiyo kanisa ndipo litaweza kukabiliana na kashfa hizo kwa nia ya kuzirekebisha.

Matukio ya kashfa dhidi ya mapadri zilianza kuvuma kwa kiwango cha juu nchini Australia na Marekani mwaka 2004,kabla ya kuibuka tena mwaka jana na kulitikisa kanisa katoliki barani Ulaya na Marekani.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/ AFP

Mhariri;Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com