1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kane avunja rekodi ya Wayne Rooney

27 Machi 2023

Timu ya taifa ya kandanda ya England inaendelea kusajili matokeo mazuri katika mechi za kufuzu kwa michuano ya Euro 2024. Cristiano Ronaldo aendelea kutamba katika rekodi ya mabao ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/4PJHN
Fußball | UEFA EURO 2020 | England - Dänemark 2021 | Harry Kane
Picha: Nick Potts/PA Images/imago images

Nahodha wa timu ya England Harry Kane alifungia tena timu yake na kusajili ushindi katika mechi za kufuzu kwa michuano ya Euro 2024 kwa kuilaza Ukraine 2-0 katika uga wa Wembley jana Jumapili.

Kane, ambaye alivunja rekodi ya ufungaji bora ya Wayne Rooney katika kikosi cha Englandkatikati mwa wiki, na  alifunga bao lake la 55 la kimataifa baada ya kupokea krosi ya Bukayo Saka dakika ya 37 ya mchezo dhidi ya Ukraine.

Dakika tatu baadaye winga wa Arsenal Bukayo Saka aliye katika kiwango kizuri kimchezo alimaliza upinzani wa Ukraine kwa kupachika wavuni bao la pili na la ushindi kwa England.

Ushindi huu unaiweka England mbele kwa pointi tatu kileleni mwa jedwali katika Kundi C baada ya kushinda nchini Italia kwa mara ya kwanza tangu 1961 siku ya Alhamisi.

SOMA PIAEuro 2022: England yaichapa Ireland Kaskazini 5-0 mechi ya mwisho ya makundi

Chini ya kocha Gareth Southgate England walisajili matokeo mazuri katika mchezo wao wa kwanza wa nyumbani tangu kushindwa vibaya na Ufaransa katika robo fainali ya Kombe la Dunia Desemba mwaka jana na bado inasubiri taji la kwanza la michuano mikubwa tangu 1966.

Mwezi Juni watarudi kwenye hatua ya kufuzu dhidi ya Malta na Macedonia Kaskazini. Timu mbili za juu katika kila kundi zitajikatia tiketi ya moja kwa moja katika michuano ya Ulaya mwakani nchini Ujerumani.

Mabingwa watetezi Italia walirejea kutoka kwa kushindwa kwao na Uingereza kwa ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Malta. Mabao yakipachikwa wavuni na mzaliwa wa Argentina Mateo Retegui na kiungo wa kati Matteo Pessina.

Ronaldo aendelea kung'ara

FIFA Fußball-WM 2022 | Portugal vs. Ghana | Tor Ronaldo
Picha: Hannah Mckay/REUTERS

Katika mechi za kundi J,  Christiano Ronaldo aliadhimisha rekodi ya mechi ya kimataifa ya 197 katikati mwa wiki na alithibitisha ubora wake wakati Ureno ilipoizaba Luxembourg 6-0 kwa kutia kimyani mabao mawili na kufikia rekodi ya mabao 122 ya kimataifa.

SOMA PIA: Kocha Martinez achukua majukumu ya Ureno

Kwingineko katika kundi J Iceland ilizinduka kutoka usingizini baada ya kulazwa na Bosnia na Herzegovina na kuicharaza Liechtenstein 7-0.  Slovakia ilisonga hadi nafasi ya pili nyuma ya Ureno kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Bosnia. 

Katika kundi H Kazakhstan ilisajili ushindi wa 3-2 dhidi ya Denmark, Slovenia kuilaza 2 bila San Marino huku Ireland Kaskazini ikipoteza moja bila dhidi ya Finland hapo jana.

Maandalizi ya kikosi cha Ujerumani

Fussball WM 2022 I DFB Training Katar
Picha: Markus Gilliar/GES/picture alliance

Nchini Ujerumani mshambuliaji Kai Havertz na beki Nico Schlotterbeck wameondolewa katika kikosi cha mechi ya kirafiki ya Ujerumani na Ubelgiji itakayochezwa mjini Cologne kesho Jumanne.

Schlotterbeck wa Borussia Dortmund alipata jeraha la msuli katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Peru siku ya Jumamosi mjini Mainz. Kai Havertz ambaye alikosa penalti dhidi ya Peru pia ataikosa mechi.

Shirikisho la Soka la Ujerumani lilisema katika taarifa kwamba hakuna mchezaji atabadilishwa katika kikosi kitakachomenyana na Ubelgiji. Kukosekana kwa Havertz kuna uwezekano wa kufungua mlango kwa Serge Gnabry.

 

//dpa,AFP