1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kandanda la England kuanza tena kutimua vumbi

Bruce Amani
15 Juni 2020

Ligi Kuu ya kandanda England, Premier League inarejea wiki hii baada ya kusitishwa kutokana na janga la corona na Liverpool huenda hivi karibuni hatimaye wakamaliza kiu yao ya miaka 30 ya kutafuta ubingwa

https://p.dw.com/p/3dnmX
Premier League - FC Liverpool v Tottenham Hotspur
Picha: picture-alliance/dpa/Actionplus

Nambari mbili Manchester City lazima waepuke kichapo dhidi ya Arsenal Jumatano wakati ligi itarudi ili kuwazuia Liverpool kuwa na fursa ya kukamilisha mambo ugenini dhidi ya mahasimu wa mjini Everton Jumapili. Aston Villa ya Mbwana Samatta itafungua pazia dhidi ya Sheffield United wakati wenyeji hao wakipambana kuepuka kushushwa daraja

La Liga yarejea kwa kishindo

Ligi Kuu ya Uhispania, La Liga nayo pia ilifungua milango yake na Real Madrid wamewawekwa shinikizo vinara Barcelona kwa ushindi wao wa 3 – 1 dhidi ya Ebar na hivyo kupunguza mwanya baina yao hadi pointi mbili. Ulikuwa mtanange wa 200 kwa Zinedine Zidane kama kocha wa Madrid na alizungumzia suala la mechi kuchezwa bila mashabiki viwanjani "Inashangaza kidogo, lakini ni kwa kila mmoja, sio sisi tu. Na wachezaji wote ni mabingwa, kwa hiyo wanajua namna ya kukabiliana na hali hiyo. Hii itaendelea hivi hadi mwisho wa msimu. Hivyo, lazima tuweke vichwani kuwa hivyo ndivyo itakavyokuwa hadi mwisho wa msimu na lazima tupambane bila kuwa na mashabiki au hata kwa kuwa na mashabiki nje ya viwanja ambao wanaweza kutupa nguvu.

Mabingwa watetezi Barcelona waliwakaanga Mallorca 4 – 0 Jumamosi. Kocha wa Barca QUIQUE SETIEN alizungumzia changamoto za kurejea ligi. "Nina uhakika mambo yatakuwa mazuri kadri mechi zitakavyoendelea kuchezwa na wakati tukiendelea kupata muda zaidi wa kucheza. Kushinda mechi hii leo kwa namna tulivyofanya na kupata matokeo hayo kunatupa ujasiri wa kuendelea kuitumia faida tuliyokuwa nayo ya kuwinda taji. Nna furaha kuwa na mwanzo wa aina hii kwa sababu ni mzuri kwetu kusonga mbele

Atletico Madrid waliendelea na msimu wao wenye matatizo kwa kutoka sare ya 1-1. Na Athletic Bilbao. Wako nafasi ya tano, pointi sawa na Getafe. Nambari nne Real Sociedad ilitoka nyuma na kulazimisha sare ya 1 – 1 na Osasuna.

Ronaldo awinda taji jingine Italia

Nchini Italia, Christiano Ronaldo huenda akaongeza taji jingine kwenye orodha yake ndefu kabatini. Fainali ya Kombe la Italia inapigwa Jumatano ambapo Juventus yake CR7 itaangushana na Napoli katika dimba la Olimpiki mjini Rome. Lakini bila mashabiki uwanjani. Kisha ligfi kuu ya kandanda ya Italia – Serie A itarejea tena Jumapili wakati mojawapo ya nchi zilizoathirika pakubwa na janga la virusi vya corona ikirejea taratibu katika hali ya kawaida.