1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KANDAHAR:Mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Taleban na Korea kusini

24 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBff

Maafisa wa serikali ya Korea Kusini wanafanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la Taleban kwa mara ya kwanza.Kundi hilo limeweka muda wa mwisho kama leo jioni kabla kuwaua mateka 23 wa Korea Kusini linalowazuia nchini Afghanistan.Hatua hiyo inatokea baada ya kundi la Taleban kueleza kuwa mateka mmoja wa Kijerumani alietekwa katika kisa chengine yuko mahututi na hatma yake bado haijulikani.

Kundi hilo linatoa wito kwa Ujerumani na Korea Kusini kuondoa majeshi yao nchini humo aidha kuachiliwa kwa wafungwa wao wanaozuiliwa na serikali ya Afghanistan.Waasi hao ni sehemu ya utawala wa Taleban uliongolewa madarakani na majeshi ya Marekani mwaka 2001.Muda wa mwisho umeshasogezwa mara mbili.

Ujumbe wa Korea Kusini unaongozwa na Balozi wake nchini Afghanistan na uliwasili mkoani Ghazni ulio kusini hapo jana.Mateka hao wanazuiliwa katika eneo hilo kwa mujibu wa mkuu wa polisi mkoani humo Alishah Ahmadzai ambaye pia anashiriki katika mazungumzo hayo.

Yapata raia 1000 wa Afghanistan wanapinga kitendo hicho cha Taliban kwani kinakiuka maadili ya dini ya kiislamu.Mwili wa Mjerumani mmoja alitekwa wiki jana katika kisa tofauti ulipatikana siku ya jumapili ukiwa na majeraha ya risasi.

Korea kwa upande wake inasisitiza kuwa itaondoa majeshi yake 200 ifikapo mwisho wa mwaka kama ilivyoafikiwa chini ya mpango wa majeshi ya muungano ya kukarabati nchi ya Afghanistan.Ujerumani inashikilia kuwa haitatimiza madai ya kundi la Taleban.Waasi hao wamekuwa wakipambana na majeshi ya Marekani na NATO tangu utawala wao kupinduliwa mwaka 2001.