1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampuni ya tumbaku yatuhumiwa kushawishi sera za afya Afrika

Grace Kabogo
14 Septemba 2021

Shirika moja linalofuatilia matumizi ya tumbaki limesema kuwa kampuni kubwa ya tumbaku ya British American Tobacco, BAT inadaiwa kufanya malipo yanayotiliwa shaka kwa nchi 10 za Afrika kwa zaidi ya miaka mitano.

https://p.dw.com/p/40IEk
Zigaretten
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Talbot

Katika ripoti mbili zilizotolewa Jumanne, shirika hilo la STOP limesema kuwa kampuni ya BAT, inadaiwa kulipa zaidi ya dola laki sita pesa taslimu, magari, malipo ya siku na michango ya kampeni kwa wanasiasa, wabunge, wafanyakazi wa umma, waandishi habari na wafanyakazi wa makampuni shindani kati ya mwaka 2008 na 2013, ili kuzishawishi sera za afya na kuwahujumu washindani wake.

Kulingana na ripoti hizo, kampuni ya BAT yenye makao yake mjini London, ilitekeleza vitendo hivyo kana kwamba iko juu ya sheria, na ililenga kuingia katika soko la vijana wa Afrika. Utafiti huo umetokana na ushahidi uliotolewa na watoa taarifa, nyaraka zilizovuja na rekodi za mahakama zilizochambuliwa na Idara ya Utafiti na Udhibiti wa Tumbaku katika Chuo Kikuu cha Bath, TCRG.

Malipo hayo ni mazoea

Mtafiti wa TCRG, Andrew Rowell amesema katika taarifa yake kwamba vitendo vya ufisadi vya kampuni ya BAT barani Afrika havikuwa kwa bahati mbaya, bali yalikuwa mazoea. ''Kuenea kwa shughuli za kijiografia, miundombinu iliyotumika na idadi ya maafisa wa ngazi ya juu waliohusika zinaonesha kuwa malipo yaliyofanywa na kampuni ya BAT yalikuwa ya kawaida na kwamba mara nyingi ushahidi ulirejeshwa London,'' alifafanua Rowell.

Utafiti huo uligundua malipo 236 yanayotiliwa shaka yaliyotolewa kwa Burundi, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Malawi, Rwanda, Sudan, Tanzania, Uganda na Zambia. Malipo hayo yalikuwa jumla ya dola 601,502. Malipo hayo yanajumuisha dola 20,000 zilizotolewa kwa kamati ya bunge ya Uganda ili kuwachunguza washindani wa BAT na takriban dola 56,000 zilizotolewa kwa mkandarasi binafsi kwa ajili ya kuanzisha vurugu katika kampuni hasimu nchini Kenya.

DW eco@africa - Malawi
Mkulima wa tumbaku MalawiPicha: DW

Nchini Afrika Kusini, kampuni ya BAT inatuhumiwa kwa kusimamia mitandao miwili ya watoa habari wanaolipwa, ikiwa inafanya kazi chini ya kivuli cha wachunguzi wanaopinga biashara haramu ili kuendesha kampeni ya kuwapinga washindani wake nchini humo.

Waandishi hao wa habari wanadaiwa kulipwa kupitia makampuni yasiyokuwa na ofisi na kadi za malipo zilizotumika zilifichwa ili zisiweze kugundulika. Ushahidi umeonesha pia kuwa kampuni ya BAT inasafirisha kimagendo sigara kutoka Afrika Kusini kwenda kwenye nchi za Afrika Magharibi.

Uchunguzi mwingine wabaini malipo ya Zimbabwe

Katika uchunguzi mwingine tofauti uliofanywa na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC na Idara ya Habari za Uchunguzi uliochapishwa Jumattau, unaonesha kuwa kampuni hiyo pia inatuhumiwa kwa kujadili malipo ya hadi dola 500,000 kama hongo kwa chama tawala nchini Zimbabwe, ZANU-PF chini ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe mwaka 2013.

Kampuni hiyo inayoendesha shughuli zake kwenye zaidi ya nchi 170 katika taarifa yake imekanusha madai ya kufanya biashara hiyo haramu. Taarifa hiyo imesema madai ya aina hiyo siyo mapya na yametolewa sana kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwa miaka kadhaa. Kwa mujibu wa BAT, Januari mwaka 2021, uchunguzi uliofanywa na ofisi inayofuatilia madai ya udanganyifu nchini Uingereza, iliisafisha kampuni hiyo kuwa haihusiki na madai kama hayo.

(AFP)