1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi habari na watetezi wa haki za binadamu wadukuliwa

Saumu Mwasimba
19 Julai 2021

NSO,kampuni ya ujasusi ya Israel yaingia kwenye kadhia ya kudukua mawasiliano ya watu duniani wakiwemo viongozi wakuu wa nchi na waandishi habari

https://p.dw.com/p/3wgY7
Israel | NSO Group
Picha: Jack Guez/AFP/Getty Iamges

Uchunguzi uliofanywa na muungano wa kimataifa wa mashirika ya vyombo vya habari umegundua kuwa kampuni moja ya Israel inayohusika na masuala ya ujasusi wa kimtandao imekuwa ikiendesha udukuzi wa kufuatilia nyendo za waandishi habari ,wanaharakati wa haki za binadamu na wapinzani wa kisiasa kote duniani.

Gazeti maarufu la Marekani The Washington Post ambalo ni mwanachama wa muungano wa kimataifa wa vyombo vya habari, uliohusika katika uchunguzi huo, limeripoti kwamba miongoni mwa waandishi habari waliodukuliwa na kampuni ya Israel inayofanya shughuli za ujasusi kwa njia ya mtandao NSO ni pamoja na waandishi habari 189, zaidi ya wanasiasa 600 na kiasi wakuu 65 wa kibiashara na watetezi 85 wa haki za binadamu pamoja na viongozi wakuu chungunzima wa nchi kote duniani.

Israel | NSO Group
Picha: Ayaka Kudo/TheYomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Shirika la Forbidden Stories lenye makao yake Paris -Ufaransaa ambalo ni shirika la habari la kujitegemea,linaloundwa na waandishi habari limefanya uchunguzi pamoja na shirika la kimataifa la haki za binadamu Amnesty International na kusambaza habari hiyo kwa mashirika mengine 16 ya habari, liligundua kwamba kuna zaidi ya watu 1,000 katika nchi 50 wanaodaiwa kuwa kwenye orodha ya kuchunguzwa na kampuni hiyo ya ujasusi wa mtandaoni NSO kwa maelekezo ya wateja wao.

Na miongoni mwa watu hao wako wandishi habari, wanasiasa, maafisa wa serikali, watendaji wakuu kwenye makampuni, watetezi wa haki za binadamu na viongozi wakuu chungunzima wa nchi.

Shirika hilo la muungano wa vyombo vya habari linavijumuisha vyombo mbali mbali vya kimataifa ikiwemo shirika la habari la Associated Press, Reuters, CNN, Wall Street Journal, Le Monde na Financial Times. Shirika la kimataifa la haki za binadamu Amnesty International limesema kwamba watafiti wake wamegundua kwamba programmu maalum ya ujasusi inayoitwa Pegasus iliwekwa kwenye simu ya mchumba wa mwandishi habari wa kisaudi Jamal Khashoggi,Hatice Cengiz,siku nne tu baada ya kuuliwa kwa mwandishi habari huyo katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul mnamo mwaka 2018.

Kampuni hiyo ya NSO huku nyuma kabla ya hapo iliwahi kuhusishwa katika matukio mengine ya kumfuatulia Khashoggi. Kampuni hiyo ya Israel ya teknolojia ya udukuzi wa mitandao hata hivyo imekanusha  kuhusika na matukio hayo kupitia barua pepe ikijibu maswali iliyoulizwa na shirika la habari la AP, na kudai kwamba haijawahi hata mara moja kuwa na orodha ya watu iliyopanga kuwadukua na wala hakuna mtu yeyote wanayemdukua.

Israel | NSO Group
Picha: Jack Guez/AFP/Getty Iamges

Aidha kampuni hiyo imetoa taarifa nyingine ikisema kwamba ripoti ya shirika la Forbidden Stories imesheheni habari za dhana zisizokuwa na ukweli na nadharia zisizokuwa na ushahidi.

Lakini uchunguzi huo uliofanywa na muungano huo wa kimataifa wa vyombo vya habari unasema kwamba uchunguzi wenye ushahidi wa data umebaini kwamba  programu ya ujasusi ya kijeshi ya kampuni hiyo yenye makao yake nchini Israel ndiyo inayotumika kudukua mawasiliano ya waandishi habari, wanaharakati wa haki za binadamu na wakosoaji wa kisiasa.

Katika orodha ya namba za simu za mkononi zaidi ya 50,000 ilizozipata, Forbiden Stories na Amnesty International,1000 zilibainika kuwa za watu waliokuwa kwenye orodha ya waliopangiwa kudukuliwa. Lakini NSO inashikilia madai yake kwamba inauza programu za ujasusi kwa mashirika ya kiserikali yaliyoidhinishwa kwa ajili ya kufuatilia magaidi na wahalifu wakubwa na wala haina uwezo wa kuingilia data za wateja wake.

Mwandishi:Saumu Mwasimba