Kampeni Tanzania zazidi kupamba moto | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kampeni Tanzania zazidi kupamba moto

Wagombea wa urais na ubunge nchini Tanzania waanza wiki ya kwanza ya mwendelezo wa kampeni baada ya tume ya uchaguzi kukamilisha kupitia rufani za wagombea ubunge na udiwani walioenguliwa awali.

Wagombea wa urais na ubunge katika uchaguzi mkuu nchini Tanzania wanaanza wiki ya kwanza ya mwendelezo wa kampeni baada ya tume ya taifa ya uchaguzi NEC kukamilisha kupitia na kuchambua rufani za wagombea wa ubunge na udiwani ambao awali walienguliwa. 

Kulingana na tume ya uchaguzi, jumla ya rufaa 616 ziliwasilishwa katika tume hiyo na zote zimeshatolewa uamuzi. Tume hiyo imesema katika rufaa zilizofika mezani kwake, 160 zilikuwa ni za ubunge na 456 zikiwa zile zilizowahusu wagombea wa nafasi ya udiwani.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa tume hiyo Dr Wilson Charles amesema wagombea wote walioshinda rufaa zao wapo huru kupanda majukwaani kuzungumza na wapiga kura.

Kutolewa uamuzi kwa rufaa hizo sasa kumefungua milango ya moja kwa moja kwa wagombea wote kuingia kwa kasi kwenye kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.

Kuanzia wagombea wa udiwani, ubunge mpaka urais wakati huu wanaonekana wakizunguka kila kona ya nchi wakiwa na ajenda za kutaka kuwavutia wapiga kura wanaofikia milioni 29 ambao wamesajiliwa na tume ya uchaguzi.

Tansania Tundu Lissu Präsidentschaftskandidat (DW/S. Khamis)

Tundu Lissu, mpinzani mkubwa wa rais John Magufuli na ambaye jina lake linatawala kwenye kampeni hizo.

Majina machache yameendelea kutawala, hatua inayobashiri mwelekeo wa uchaguzi.

Uchaguzi huu ambao ni wa sita kufanyika tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992, unawajumuisha wagombea 15 wanaowania nafasi ya urais, idadi ambayo pia inatajwa kushuhudiwa kwa mara ya kwanza kwa kuwa na wagombea wengi.

Ingawa kumekuwa na idadi hiyo kubwa ya wagombea ni majina machache tu ya wagombea ndiyo yanayotawala zaidi kwenye majukuwaa ya kampeni hali ambayo imewafanya wafuatilia wa masuala ya siasa kuanza kubashiri mwelekeo wa uchaguzi huu.

Kwenye majukwaa ya kampeni nako ingawa wagombea wamejiweka kando na utumiaji wa lugha zinazoweza kutibua hali ya kisiasa, hata hivyo hawajaacha kupeana vijembe kwa kukosoana waziwazi na kushutumiana.

Tazama vidio 01:33

Queen Sendiga: Mwanamke anayewania urais Tanzania

Hata hivyo tume ya haki za binadamu na utawala bora inaona kwamba tofauti na miaka ya nyuma kampeni za mwaka huu zimetawaliwa na weledi mkubwa.Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema hadi sasa tume hiyo haijarekodi visa vyovyote vinavyohusiana na uvunjifu wa haki za binadamu.

Miongoni mwa mambo yanayotiliwa mkazo karibu na wagombea wote ni pamoja na yale yanayohusu uboreshaji wa sekta ya afya kwa kuanzisha bima za afya, kutumia rasilimali za nchi kuharakisha maendeleo ya uimarishaji wa huduma kama umeme, elimu na ushirikiano wa kikanda.

George Njogopa- Dar es Salaam.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com