1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA:Wanasheria wajiunga na mgomo wa majaji

7 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCLQ

Wanasheria nchini Uganda wanapanga kugoma wiki ijayo ili kuunga mkono majaji waliogoma kufuatia kukamatwa tena kwa wafuasi wa upinzani katika mahakama kuu waliokuwa wameachiwa kwa dhamana.

Majaji nchini humo walianza mgomo wa wiki moja siku ya Jumatatu ili kupinga uvamizi kinyume na sheria wa mahakama kuu Alhamisi iliyopita.Maafisa wa polisi waliojihami kwa silaha walivamia mahakama hiyo na kuwakamata tena wafuasi sita wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change ,FDC kinachoongozwa na Kizza Besigye.Aidha polisi hao waliharibu samani ya mahakama hiyo na kumpiga mwansheria mmoja hadi kuzirai.

Watu hao sita walishtakiwa kwa kupanga njama ya kupindua serikali pamoja na kiongozi mkuu wa Upinzani Kizza Besigye.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda alifanya mkutano na Jaji mkuu Benjamin Odoki na kutoa taarifa iliyounga mkono vitendo vya mapolisi hao.Kwa upande mwingine Rais Museveni alishtumu majaji nchini humo kwa kuwaachia watu hao sita kwa dhamana wanaoshukiwa kwa kosa la uhaini.