1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamishina Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu

Othman, Miraji7 Agosti 2008

Raia wa Afrika Kusini ni msimamizi mkuu wa haki za binadamu duniani

https://p.dw.com/p/EsI9
Bibi Naventhem Pillay, kamishina mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za BinadamuPicha: dpa Zentralbild

Uzoefu na misukosuko anayoipata mtu maishani mara nyingi humfanya mtu huyo awe namna alivyo. Na hivyo ndivyo ilivyo kwa Bibi Naventhem Pillay wa kutoka Afrika Kusini ambaye kutoka Septemba Mosi, mwezi ujao, atakua kamishina mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu. Bibi huyo, ambaye sasa ana umri wa miaka 67, aliishi chini ya mfumo wa ubaguzi wa rangi katika nchi yake, na huko ndiko alipojionea namna haki za binadamu zinavoweza kupondwa.

Kazi hii kubwa ya kuwa kamishina mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu inaambatana na kuendeleza na kulinda haki za binadamu. Kuna watu walio na wasiwasi kama Bibi Pillay atakua mkakamavu kama mtangulizi wake, Louise Arbour, katika kuziandama tawala za kiimla, zikiwemo zile zilioko katika bara lake la Afrika. Ban -Ki Moon, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, mtu aliyemteua, anatarajia kwamba atabakia mtu anayejitegemea, kama vile anavotakiwa mtu anayeshika wadhifa huo.

Mwandishi wa habari Nicodamus Ikonko, anamkumbuka kama hivi Bibi Pilly alipokuwa jaji katika mahakama ya kimataifa ya Arusha iliosikiliza kesi za mauaji ya kiholela ya Rwanda ya mwaka 1994:

Bibi Mary Robinson, kamishina mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za Binadamu anayetokea Ireland, ambaye alizikosoa nchi kama vile Marekani, China na Israel kwa kwenda kinyume na sheria za kiutu na uhuru wa raia, alilazimika kujiuzulu baada ya miezi 12 ya mkataba wake kurefushwa kwa miaka minne kwa vile kulikuweko nchi kadhaa zilizompinga. Bibi Riobinson alikua anazungumza wazi juu ya malalamiko yake na hata akazilaumu sana nchi za Magharibi juu ya uhalali wa kuishambulia kwa mabomu Yogoslavia ya zamani kulikofanywa na ndege za Shirika la Kujihami la Kambi ya Magharibi, NATO, jambo ambalo lilipelekea raia kuuwawa

Bibi Pillay atachukuwa mahala pa Louise Arbour, ambaye zamani alikuwa jaji katika mahakama kuu ya Kanada. Pia Louise Arbaour alikua hataki mchezo linapokuja suala la haki za binadamu na alikataliwa kuingia Korea Kaskazini na Myanmar. Pale alipotembelea Sri Lanka mwanzoni mwa mwaka huu, aliulizwa huko na maafisa kwa nini hatembelei jela Kimarekani la Guantanamo. Na pale alipokutana na wabunge wa Kimarekani, walimgeuzia kibao na kumuuliza kwanini hatembelea Mnyanmar ambayo serekali ya nchi hiyo mara kadhaa imelaumiwa na Umoja wa Mataifa kwa kwenda kinyume na haki za binadamu.

Mwezi uliopita Navanethem Pillay aliteuliwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon kushika wadhifa huo mpya; uteuzi huo ulikubaliwa na wanachama katika kikao cha Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Bibi Pillay ni wa kutoka jamii ya Watamil huko Afrika Kusini, akitokea katika tabaka ya chini, baba yake akiwa ni dereva wa basi. Alianza kazi yake ya uwakili kwa kuwatetea wapinzani wa utawala wa wa ubaguzi wa rangi. Nilimuuliza mwandishi wa habari Issac Khomu kama ni kawaida kwa watu wa tabaka ya chini, tena akiwa wa asili ya Kiasia, kupanda juu katika nyadhifa huko Afrika Kusini:

Baadae alitumikia Mahakama ya Umoja wa Mataifa iliokuwa inasikiliza kesi za wale watu walioendesha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, na kuwa mwenyekiti wa jopo la majaji lililomhuku waziri mkuu wa zamani wa Rwanda kwa kuhusika na mauaji ya kimbari na kumpa kifungo cha maisha gerezani.

Nicodamus Ikonko, mwandishi wa habari aliyefuata kesi ya mauaji ya Rwanda katika mahakama ya kimataifa mjini Arusha, alikuweko pale Jaji Naventhem Pillay alipotoa hukumu hiyo:

Baadae Bibi Pillay alikua jaji katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya mjini The Hague.

Katika mahojiano, Bibi Pillay alitilia mkazo juu ya maendeleo yaliofanyika katika kuzitukuza haki za bi nadamu duniani kote, akiashiria kuanzishwa Baraza la Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu kuwa ni mfano wa namna nchi zinavowekea umuhimu masuala ya haki. Alisema uzoefu wake mzuri kama hakimu wa kimataifa ni pale uongozi wa kisiasa unapotakiwa ujielezee namna ulivoshiriki katika vitendo vibaya sana vya kihalifu, kama vile mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya uutu na wa vita. Bibi huyo alikua katika jopo la majaji waliomhukumu waziri mkuu wa zamani wa Rwanda na kumpa kifungo cha maisha gerezani kwa kumpata na na hatia ya mauaji ya kimbari.

Bibi Pillay, aliyesomea sheria katika vyuo vikuu vya Natal, Afrika Kusini, na Havard, Marekani, alisema kuundwa mahakama za kimataifa za uhalifu mnamo miaka 15 iliopita, kukiwemo ile mahakama ya kimataifa ya jinai, ICC, kumetoa ishara wazi kwamba hakutakuweko kinga na kwamba mtu yeyote, kama ni mkuu wa nchi au kiongozi wa wanamgambo, atatakiwa awajibike na aadhibiwe pindi atapatikana na hatia. Lakini anatambua kwamba kazi yake mpya itahitaji mbinu zaidi za kidiplomasia kuliko zile za kijaji. Yeye anajua thama kwamba kesi za uhalifu zina nguvu za kuadhibu, lakini kamishina mkuu wa haki za binadamu anabidi atumie njia mbali mbali za kushawishi, kuzungumza kwa nguvu au kuendeleza jumuiya za kiraia ili zikabiliane na vyanzo vya vitendo vya kuendewa kinyume haki za binadamu. Anachukuwa wadhifa huo wakati Umoja wa Mataifa unaadhimisha mwaka wa 60 tangu kutolewa lile tangazo la dunia juu ya haki za binadamu na wakati Baraza la Usalama la umoja huo limekwama juu ya masuala ya haki za binadamu katika Sudan, Zimbabwe, Mnyanmar na katika ardhi za Waarabu zilizotekwa na Israel. Mkataba wake utakua wa miaka minne na makao yake yatakua Geneva akiwasimamia wafanya kazi zaidi ya 1,000 waliotapakaa katika nchi 50 na bajeti ya zaidi ya dola milioni 150 kila mwaka.

Lakini imekuwaje jamii ya kimataifa ikamchagua raia wa Afrika Kusini kwa kazi hiyo muhimu, lakini ilio ngumu pia. Mwandishi wa habari wa huko Johannesburg, Issac Khomu aliniambia hivi:

Kwa hayo basi ndio nakamilisha makala haya ya Mbiu ya Mnyonge, maakala juu ya haki za binadamu, iliowajia kutoka Deutsche Welle, mjini Bonn, Ujerumani. hadi mara nyingine ni Othman Miraji...