1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatisha kujiondoa

Admin.WagnerD27 Novemba 2015

Kamati ya muungano wa nchi zilizosaini mkataba wa Roma ulioianzisha Mahakama ya ICC, imelikubali ombi la Kenya la kukifanyia marekebisho kifungu cha 68 cha sheria katika kesi inayomkabili makamu wa rais William Ruto.

https://p.dw.com/p/1HDP6
William Ruto
Picha: Michael Kooren/AFP/Getty Images

Baada ya siku kadhaa za mashauriano katika kikao cha 14 cha mataifa yaliyosaini mkataba wa Roma ulioiunda mahakama ya ICC, jana (26.11.2015) Kenya ilifanikiwa kupata azimio ambayo yumkini linaweza kufutilia mbali matumizi ya ushahidi wa kurekodiwa katika mahakama ya kimatiafa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague. Kenya ilishinikiza ushahidi wa kurekodiwa usitumike katika kesi inayomkabili makamu wa rais William Ruto na mwandishi wa habari Joshua Sang.

Taarifa ya mkutano huo ilisema azimio la mahakama ya ICC la Novemba 27 mwaka 2013 liloifanyia marekebisho sheria ya 68 ya Sheria ya Utaratibu na Ushahidi limesitishwa. Kenya iliikubali taarifa hiyo baada ya sentensi iliyosema "Sheria ya 68 iliridhiwa na kuanza kutumika kuanzia Novemba 27,2013." kufutwa.

Lakini Ruto na Sanga itabidi wasubiri matokeo ya rufaa waliyoiwasilisha katika mahakama ya ICC kuhusu utumiaji wa ushahidi uliorekodiwa wa mashahidi watano. Sheria hiyo inaruhusu ushahiri uliorekodiwa awali utumike, ilimradi mwendesha mashtaka na upande wa utetezi ulimhoji shahidi wakati kesi ilipokuwa ikisikilizwa, kama shahidi hawezi kufika mahakamani. Kama yupo mahakamani, sheria inataka shahidi akubali ushahidi wake alioutoa awali na kurekodiwa utumike, na upande wa waendesha mashtaka, utetezi na majaji wamuhoji wakati kesi itakapokuwa ikisikilizwa.

Hapo kabla Kenya ilisema iko tayari kujiondoa kutoka mahakama ya kimataifa ya ICC ikiwa haitapata hakikisho kuhusu jinsi kesi inayomkabili Ruto itakavyoendeshwa, kauli ambayo inazidisha tofauti kati ya mataifa ya Afrika na mahakama hiyo.

Makamu wa rais William Ruto anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo mauwaji, kuwahamisha watu kwa nguvu na mateso kufuatia vita vya kikabila baada ya uchaguzi wa Rais wa 2007.

Kenya yataka hakikisho

Mawakili wawili wakuu wa serikali wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Kenya ilitaka kuhakikishiwa kuwa sheria mpya inayoruhusu mahakama kutumia ushahidi kutoka kwa mashahidi ambao wameamua kujiondoa kwenye kesi haitatumika kwa kesi kama ya Ruto. Wakili huyo amesema kujiondoa kutoka mahakama hiyo ya kimataifa ndio suluhisho pekee lililopo kwa Kenya ikiwa ombi lao halitasikilizwa.

Kenia Prozess gegen William Ruto in Den Haag Fatou Bensouda
Kiongozi mkuu wa mashtaka ICC Fatou BensoudaPicha: Reuters

Maafisa wa serikali ya Kenya walitaka hakikisho hilo hapo jana kwenye mkutano wa shirika la mahakama hiyo ya The Hague. Wanachama hao hawakuweza kuthibitisha ikiwa wako tayari kujiondoa mara moja iwapo matakwa yao hayataafikiwa kwenye mkutano huo.

Kenya itakuwa taifa la kwanza kati ya nchi wanachama 123 wa mahakama hiyo kujiondoa tangu kuanza kwa mahakama hiyo mwaka 2002 iliyokusudiwa kumaliza mtindo wa viongozi kutojali sheria kwa kutenda uhalifu wa kivita, dhidi ya binadamu au mauwaji ya halaiki.

Mataifa ya Afrika yadai Kenya imeonewa

Umoja wa Afrika na Mataifa mengine yameilaumu mahakama ya ICC kwa kuyaonea mataifa ya Afrika haswa katika kesi inazozishughulikia sasa. Lakini madai hayo yamekanushwa na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo, Fatou Bensouda.

Wakili wa Nairobi George Kithi amesema swala la kujiondoa linaweza kushughilikiwa mahakamani.

Viongozi wa mashtaka katika mahakama ya ICC walilazimika kutupilia mbali mashtaka dhidi ya Rais Wa Kenya Uhuru Kenyatta, ambaye walimlaumu kwa kuchochea mapigano ya kikabila baada ya uchaguzi. Walilaumu muingilio wa kisiasa kwa mashahidi haswa baada ya Kenyatta kuchaguliwa Rais mwaka 2013 kuwa sababu ya kutoendelea kwa kesi dhidi ya rais huyo. Kenyatta amekana madai hayo.

Wizara ya maswala ya nchi za kigeni ya Kenya ilisema kwenye mtandao wa twita kutoka The Hague kuwa Kenya haina njia nyingine kulingana na hali ilivyo ila kuamua kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo iliyoundwa kutokana na mkataba wa Roma.

Kenya na Afrika kusini zilikuwa zimeshirikiana kuyashawishi mataifa mengine katika kutaka kuwepo uhuru zaidi wa tafsiri ya sheria za mahakama hiyo.

Mwandishi:Bernard Maranga/Reuters
Mhariri:Josephat Charo