1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamati Kuu ya FIFA yaidhinisha mageuzi

4 Desemba 2015

Viongozi wa kandanda walikuwa kwenye mkutano wakijadili namna ya kuleta mageuzi katika shirikisho hilo ambalo limetumbukia gizani kutokana na kashfa ya ufisadi

https://p.dw.com/p/1HHa8
Zürich FIFA Interims-Präsident Issa Hayatou
Picha: Getty Imgages/AFP/F. Coffrini

Kamati Kuu ya FIFA ilikubaliana kwa kauli moja mpango wa mageuzi ambao ni pamoja na kuwekea kikomo muhula wa urais kwa hadi miaka 12. Hata hivyo hapatakuwa na suala la kuuwekea kikomo umri wa wagombea wa wadhifa huo. Mageuzi mengine yaliyoidhinishwa ni pamoja na kuweka uwazi katika mishahara ya maafisa wa kandanda. RANCOIS CARRARD, ni mwenyekiti wa kamati ya mageuzi ya FIFA "Kama ninavyosisitiza huu ni mwanzo wa mchakato wa mageuzi. Sheria hizi zinaweza kulinganishwa na kile nnachosema ni treni ambayo inaondoka kituoni huku injini zake zikinguruma na treni hiyo iko barabarani. Kituo kinacofuata, kituo cha kwanza, kitakuwa muhimu sana, Baraza Kuu, na kutakuwa na vituo vingine kadhaa katika barabara hiyo ya treni. Kile ninachotaka pia kusisitiza ni namna kamati kuu ilivyoidhinisha kwa kauli moja mpango huu mzima wa mageuzi tuliouwasilisha".

Mpango huo wa mageuzi lazima uidhinishwe na mashirikisho 209 wanachama katika mkutano mkuu wa FIFA unaopangwa Februari 26 mwakani.

Platini na Blatter kujua hatma yao

Tukibakia na kandanda la kimataifa ni kuwa Sepp Blatter na Michel Platini wanatarajiwa kufika mbele a kamati ya maadili ya FIFA katika kipindi cha wiki mbili zijazo kujibu tuhuma za rushwa.

Duru zinasema kuwa vikao vya kusikiskizwa kesi za viongozi hao waliosimamishwa uongozi kutokana na madi ya rushwa, vitaandaliwa Desemba 16 hadi 18 mjini Zurich, Uswisi. Uamuzi kisha utachukuliwa baada ya siku chache.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/reuters
Mhariri: Josephat Charo