1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame 'kushinda' kwa kishindo

Mohammed Khelef
4 Agosti 2017

Wanyarwanda wamepiga kura katika uchaguzi unaotarajiwa kumpa ushindi wa kishindo rais wa kipindi kirefu nchini humo Paul Kagame, aliyekwishasema kuwa siku ya uchaguzi wa urais itakuwa ada tu.

https://p.dw.com/p/2hiip
Kagame, Rwanda, Kigali, uchaguzi
Picha: Reuters/J. Bizimana

Rais Kagame yupo katika mbio hizi za kuwania urais na Frank Habineza  wa chama cha Democratic Green Party of  Rwanda ambacho ndio chama pekee cha upinzani nchini humo kilichosajiliwa. Mgombea wa kujitegemea, Philippe Mpayimana, mwandishi habari wa zamani pia anawania nafasi hiyo. 

Kumekuwepo na mistari mirefu ya wapiga kura nje ya vituo vya kupigia kura katika baadhi ya maeneo mjini Kigali. Rais Paul Kagame hakusema lolote baada ya kupiga kura yake katika shule moja ya msingi. Mpayimana na Habineza walipiga kura katika maeneo mengine mjini humo. 

Katika uchaguzi huu wagombea watatu wengine walipigwa marufuku kushiriki zoezi hilo na tume ya uchaguzi kwa kushindwa kutekeleza mahitaji Fulani ikiwemo kupata sahihi za kutosha za kuwawezesha kugombea.

Aidha katika vituo vyengine vya kupigia kura kulikuwepo na miziki iliyokuwa ikiwashawishi wapiga kura kumchagua kiongozi atakayeibadilisha nchi na kuwaunganisha wanyarwanda wote.

"Hata wakosoaji watakwambia Kagame ni kiongozi wa kipekee anayefanya mambo kwa vitendo," alisema mkaazi wa Kigali, Charles Karemera, mara tu baada ya kupiga kura yake.

Paul Kagame, Rwanda, Kigali
Rais Paul Kagame akipiga kura yake mapema asubuhi ya Agosti 4, 2017Picha: E. Gatanazi

Vituo ya kupigia kura vilifungwa saa tisa mchana huku matokeo ya mwanzo yakitarajiwa kutolewa baadaye leo jioni hii ikiwa ni kwa mujibu wa katibu mtendaji wa tume ya uchaguzi ya Rwanda Charles Munyaneza.

Kagame, aliye na miaka 59, ameiongoza Rwanda iliyo na idadi ya watu milioni 12 kuanzia mwaka wa 1994 baada ya kumalizika vita ya kimbari vilivyosababisha mauaji ya watu 800,000 kutoka kabila wa watutsi na wahutu.

Hata hivyo, rais huyo amebakia kuwa maarufu kufuatia juhudi zake za kuinua uchumi wa nchi lakini wakosoaji wanadai kiongozi huyo anatumia madaraka yake kuukandamiza upinzani. 

Serikali ya Rwanda akiwemo Kagame mwenyewe imekanusha madai ya wakosoaji kwamba serikali inalenga wapinzani kwa mauaji au kutoweka.

Aidha kura ya maoni iliyofanyika mwaka wa 2015 ilimruhusu Kagame kubakia madarakani mpaka mwaka wa 2034 iwapo ataamua kufanya hivyo.

Wapiga kura milioni 6.9 walisajiliwa kupiga kura huku zaidi ya Wanyarwanda 44,000 waishiyo nje ya nchi wakipiga kura zao hapo jana. 

Mwandishi: Amina Abubakar/AP 
Mhariri: Mohammed Khelef