1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa UEFA Platini amtaka Blatter kujiuzulu

Admin.WagnerD28 Mei 2015

Rais wa Shirikisho la kandanda la Ulaya – UEFA, Michel Platini amemtaka Rais wa FIFA, Sepp Blatter kujiuzulu kwa sababu ya kashfa za ufisadi zinazolikumba kandanda la kimataifa.

https://p.dw.com/p/1FXuw
Zürich UEFA Pressekonferenz Michel Platini Korruptionsskandal
Picha: Reuters/R. Sprich

Platini ameyataka mataifa wanachama wa FIFA kumuunga mkono Mwanamfalme wa Jordan Ali bin al Hussein katika uchaguzi wa kesho ambapo Blatter anatarajiwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa tano. Bruce Amani na matukio ya hivi punde.))

Platini amekutana ana kwa ana na Blatter katika mkutano wa dharura wa wakuu wa kandanda akimtaka ajiuzulu kwa sababu ya kashfa za rushwa. Blatter alikataa wito huo na kisha Platini akatoa tamko kwa vyombo vya habari akiwataka mataifa wanachama kutoka kote ulimwenguni kupiga kura ya kumpinga Blatter katika uchaguzi wa urais wa hapo kesho."tulikwenda katiak ofisi yake na nikarudia ushauri wangu kwake aondoke na kuwa anastahili kujiuzulu. Kwamba anastahili kugundua kuwa muda huu sio mzuri kwake. Na awe na ujasiri na uaminifu wa kugundua kuwa mambo siyo mazuri. Na aliniambia Michel, tunajuana sana, lakini muda ushapita. Siwezi kuondoka wakati mkutano wa baraza kuu unaanza jioni hii. Nikamwambia, bwana rais, hiyo ni aibu. Nadhani ingekuwa vyema kwa sifa yako ikiwa ungetuacha sasa".

Platini amesema amesikitishwa na matukio ambayo yalisababishwa kukamatwa maafisa saba wa FIFA katika hoteli moja ya mjini Zurich jana Jumatano.

Mkutano wa baraza kuu la FIFA unaendelea mjini Zurich
Mkutano wa baraza kuu la FIFA unaendelea mjini ZurichPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Blatter anaonekana na wengi kuwa atashinda uchaguzi huo na kuongoza kwa muhula wa tano, lakini Platini anasema anaamini kuwa Mswisi huyo ataweza kushindwa. Amesema idadi kubwa ya mataifa ya Ulaya yatamuunga mkono mpinzani wa Blatter, Mwanamfalme wa Jordan Ali bin al Hussein, na kuyaomba mashirikisho mengine pia kujiunga katika vuguvugu la kuipinga FIFA.

Mshindi atahitaji theluthi mbili ya wingi wa kura kutoka kwa wanachama 209 wa FIFA ili kupata ushindi katika duru ya kwanza. Ikiwa duru ya pili itahitajika, ushndi wa moja kwa moja utatosha.

Rais wa Urusi Vladmir Putin ameitetea haki ya Urusi kuandaa Kombe la Dunia mwaka wa 2018 huku akiikosoa Marekani kwa kuyaingilia masuala nje ya mipaka yake ya kisheria baada ya kuamuru kukamatwa maafisa wakuu wa FIFA.

Putin amesema kitendo cha kukamatwa maafisa wa FIFA nchini Uswisi hapo jana ni “jaribio la wazi” la kuzuia kuchaguliwa tena kwa mkuu wa FIFA Sepp Blatter.

Wakati huo huo, Waziri wa Michezo wa Afrika Kusini Fikile Mbalula amekanusha tuhuma kuwa kiasi kikubwa cha hongo kilitolewa ili kupata kibali cha kuandaa Kombe la Dunia la 2010, akisema kuwa fedha za umma hazikuwahi kutolewa kwa “wahalifu”

Nyaraka za Marekani zinaonyesha kuwa serikali ya Afrika Kusini ilikubali kuwa dola milioni 10 zilizostahili kulipwa na nchi hiyo ili kuandaa Kombe la Dunia badala yake zilihamishwa kutoka kwa hazina ya FIFA ili kutoa hongo kwa aliyekuwa makamu wa rais wa FIFA Jack Warner.

Maafisa wa Uswisi wanasema kuwa watu wote saba waliokamatwa na kuzuiliwa mjini Zurich kwa tuhuma za rushwa watapinga kupelekwa Marekani.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFPE/reuters
Mhariri: Mohammed Khelef