1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kabore ni rais mteule wa Burkina Faso

1 Desemba 2015

Waziri mkuu wa zamani wa Burkina Faso, Roch Marc Christian Kabore, ameshinda uchaguzi wa Rais uliofanyika mwaka mmoja baada ya Blaise Compaore kutolewa madarakani kufuatia maandamano ya kumpinga.

https://p.dw.com/p/1HF7s
Burkina Faso Wahl in Ouagadougou Präsdentschaftskandidat Roch Marc Kabore
Picha: Reuters/J. Penney

Hakuna aliyetarajia matokeo ya wazi katika uchaguzi wa Burkina Faso. Katika duru ya kwanza mgombea wa chama cha Movement of People for Progress, MPP, Roch Marc Christian Kabore mwenye umri wa miaka 58 amechaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita wakati Wabukinabe walipojitokeza kumchagua rais baada ya kipindi cha miaka 27.

Akiyatangaza matokeo hayo, Mkuu wa tume huru ya kitaifa ya uchaguzi, CENI, Barthelemy Kere, amesema Kabore ameshinda kwa asilimia 53.49 ya kura na kuwapongeza wagombea. "Nawapongeza wagombea wote walioshiriki katika uchaguzi huu. Wote ni washindi kupitia kampeni zao, haki, uvumilivu wao na heshima walioonyesha kwa kila mmoja."

"Lazima turejee kazini mara moja. Kwa pamoja tunatakiwa kulihudumia taifa," amesema Kabore wakati alipowahutubia maelfu ya wafuasi wake nje ya makao makuu ya chama chake na kuahidi kufanya juhudi za dhati kuhakikisha fursa zinapatikana kwa mustakabali mwema wa siku za usoni.

Kabore aidha alisema, "Ili kujitolea kwetu kusiwe kazi bure, lazima tufanye juhudi kuponya majeraha na kupata ukweli na haki, maridhiano ya kitaifa na kuimarisha mshikamano wa kijamii miongoni mwa Wabukinabe wote."

Wanasiasa, waandishi wa habari na waangalizi wa uchaguzi waliyasubiri matokeo hayo kwa saa kadhaa kabla kutangazwa muda mfupi baada ya saa sita usiku.

Burkina Faso Präsidentschaftswahlen Zephirin Diabre
Zephirin Diabre akipiga kura OuagadougouPicha: DW/K. Gänsler

Ushindi wa Kabore katika duru ya kwanza ya uchaguzi ulianza kuonekana wakati kura zilipokuwa zikiendelea kuhesabiwa hapo jana. Hata hivyo umeelezwa kuwa wa kushangaza kwa kuwa wiki chache zilizopita waangalizi walikuwa na msimamo wa pamoja kwamba kungefanyika duru ya pili ya uchaguzi.

Mpinzani mkuu wa Kabore, Zephirin Diabre, wa Muungano wa Maendeleo na Mageuzi, Union for Progress and Change, UPC, anashika nafasi ya pili kwa kushinda asilimia 21.65 ya kura.

Diabre, waziri wa zamani wa fedha wa Burkina Faso aliyewahi pia kufanya kazi na Umoja wa Mataifa, amempongeza Kabore kupitia akaunti yake katika mtandao wa Twitter na baadaye kibinafsi, muda mfupi kabla matokeo ya mwisho rasmi kutangazwa.

Uchaguzi wapongezwa

Wagombea 14 walichuana katika kinyang'anyiro cha urais na kuufanya uchaguzi huo kuwa vigumu kubashiri mshindi. Hata hivyo uchaguzi huo umepongezwa kwa kuandaliwa na kufanyika vizuri.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, kupitia msemaji wake Stephane Dujarric, amesifu jinsi uchaguzi ulivyofanyika katika mazingira ya amani na kushiriki kwa idadi kubwa ya wanawake katika mchakato wa uchaguzi.

Ban amewahimiza viongozi wote wa kisiasa na wadau kuendeleza mazingira ya amani ya siku ya uchaguzi na kutaka mizozo yote itatuliwe kwa njia za kisheria.

Wabukinabe wana matumaini uchaguzi huu utaleta enzi mpya ya demokrasia ya amani na wanasubiri kuona ikiwa kweli rais mteule Kabore ataleta mageuzi yanayotarajiwa. Wakosoaji wanasema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 58 ana mafungamano ya karibu sana na utawala wa kiongozi zamani, Blaise Compaore. Kabore alikuwa waziri mkuu kuanzia 1994 hadi 1996 na kuanzia 2002 akawa spika wa bunge kwa miaka kumi. Lakini Kabore hataki kuwa muwakilishi wa mfumo wa zamani wa Compaore.

Ushindi wa Kabore unakuja mwaka mmoja baada ya machafuko yaliyosababisha Compaore kuondolewa madarakani Oktoba mwaka uliopita alipojaribu kuurefusha utawala wake wa miaka 27 kwa kuibadili katiba. Burkina Faso ilitumbukia tena katika machafuko Septemba mwaka huu wakati kikosi maalumu cha ulinzi wa rais kilipojaribu kuchukua madaraka kutoka kwa serikali ya mpito iliyoongozwa na rais Michel Kafando kupitia mapinduzi, na kusababisha uchaguzi kuahirishwa.

Mwandishi: Katrin Gänsler

Tafsiri: Josephat Charo

Mhariri: Caro Robi