1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kabila na Tshisekedi wakubaliana muundo serikali ya mseto

Angela Mdungu
30 Julai 2019

Hatimaye Rais Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila wamekubaliana kuhusu muundo wa serikali ya mseto ambayo itakuwa na mawaziri na manaibu waziri 65.

https://p.dw.com/p/3Mxpj
DR Kongo scheidender Präsident Joseph Kabila neben Nachfolger Felix Tshisekedi während einer Einweihungsfeier in Kinshasa
Picha: Reuters TV

Wajumbe kutoka pande mbili hizo wametia saini mkataba rasmi wa ugavi wa madaraka, ambao wamesema kutakuweko na kamati ya ufuatiliaji wa mkataba huo. Serikali imetarajiwa kutangazwa mnamo wiki mbili zijazo. 

Kusainiwa kwa mkataba huo kumefanyika saa sita, usiku wa kuamkia leo baada ya siku kadhaa za mazungumzo ambayo hayakuwa mepesi amesema Nehemie Mwilanya, aliyeliwakilisha vuguvugu la FCC la Joseph Kabila kwenye mazungumzo hayo.

Mwinyala amesema Rais Tshisekedi na  Kabila walionyesha uzalendo ili kufikia sio tu mageuzi ya mani kwenye uongozi wa taifa bali pia makubaliano hayo kwa ajili ya serikali ya muungano baina ya vuguvugu la FCC na lile la CASH kufuatia mazungumzo marefu.

Mkataba huo wa kuweko na serikali ya mseto unaelezea kwamba baraza la mawaziri litakuwa na jumla ya mawaziri 65. FCC ya Kabila itachukuwa mawaziri 42 na CASH ya Rais Tshisekedi wizara 23. Hata hivyo mkataba huo haukufafanua ni wizara gani kila upande utachukua.

Duru zinaelezea kwamba Rais Tshisekedi atamteua waziri wa mambo ya ndani, waziri wa mambo ya nje, huyo wa bajeti na uchumi na gavana wa benki kuu, huku Joseph Kabila akipewa mbali na waziri mkuu, wizara ya ulinzi, sheria, fedha na akiba.

Lengo la serikali ya pamoja latajwa

Jean-Marc Kabund A Kabund, kiongozi wa muda wa chama cha UDPS na aliyemuwakilisha Rais Tshisekedi kwenye mazungumzo hayo amesema kwamba lengo la serikali hiyo ya mseto ni pamoja na kuendesha mageuzi ya sekta ya sheria na uchumi.

Kabund amesema mkataba huo unazingatia mikakati itakayomuongoza waziri mkuu katika kuunda baraza lake la mawaziri ambalo litaidhinishwa na Rais.

DR Kongo Präsident Kabila einigt sich mit Opposition Felix Tshisekedi
Picha: Reuters/K. Katombe

Ni miezi sita sasa tangu kuapishwa kwa Rais Tshisekedi,lakini hakujakuweko na serikali mpya. Waziri mkuu Sylvestre Ilunga aliyeteuliwa Mei 20 alishindwa kuunda serikali. Alitakiwa kusubiri hadi kuwepo na makubaliano ya ugavi wa madaraka ili kuteua baraza lake la mawaziri.

Katiba ya Kongo inaelezea kwamba chama chenye wingi wa viti bungeni ndicho kinamteua waziri mkuu. Vuguvugu la FCC la Rais mstaafu Joseph Kabila ndilo limeshikilia wingi wa viti bungeni na pia kwenye baraza la seneti.

Jumamosi iliyopita, Alexis Thambwe Mwamba aliyekuwa waziri wa sheria ndiye aliyechaguliwa kuwa spika wa seneti. Hii leo viongozi wa upinzani wa vuguvugu la LAMUKA wanatarajiwa kukutana mjini Lubumbashi ili kutoa msimamo wao kuhusu hali ya kisiasa nchini.

Mkutano huo utakaoongozwa na Moise Katumbi, umehudhuriwa pia na Martin Fayulu na Adolphe Muzito. Kutokana na matatizo ya kiufundi ya ndege yake, Jeanpierre Bemba alielezea kwamba hatohudhuria mkutano huo huku akiwakilishwa na Eve bazaiba katibu mkuu wa chama chake cha MLC.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo (Kinshasa)