1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KÖLON : Mkutano wa Kanisa la Kiprotestanti waanza leo

6 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBuN

Mkutano wa 31 wa kila mwaka wa kanisa kuu la madhehebu ya Kiprotestanti nchini Ujerumani umeanza katika mji wa Cologne leo hii.

Zaidi ya washiriki 100,000 wa Ujerumani wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo pamoja na wageni 4,000 kutoka nje.

Mwenyekiti wa Kanisa la Kiprotestanti nchini Ujerumani Askofu Wolfgang Huber amesema mkutano huo wa siku tano unakusudia kujenga mahusiano na mkutano wa Kundi la Mataifa Manane yenye Maendeleo makubwa ya viwanda duniani unaofanyika kwa wakati mmoja huko Heiligendamm.

Mkuu wa Kanisa la Kiprotestanti katika mkoa wa Rhienland Nikolaus Schneider amesema ujumbe wao kwa viongozi hao wa Kundi la G8 utakuwa wa kuwasisimuwa kidogo kwa viongozi hao kwani hawawezi kuendelea kuishi katika dunia ambayo ina uwezo wa kuwalisha vizuri watu wote lakini hata hivyo bado kuna watu milioni 800 wanaokabiliwa na njaa na kila siku watoto 10,000 wanakufa jambo ambalo lingeliweza kuepukwa.

Amesema hizo ni kashfa kubwa ambazo zinaweza kuzuiliwa na jamii kwani uwezo wanao.

Mada kuu katika mkutano huo wa Kanisa la Kiprotestanti nchini Ujerumani itakuwa ni utandawazi,vita dhidi ya umaskini duniani na mdahalo na Waislamu.

Mkutano huo unamalizika tarehe 10 mwezi wa Juni.