Jumuiya ya Kimataifa yatiwa khofu na kura ya maoni ya Sudan ya Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.09.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jumuiya ya Kimataifa yatiwa khofu na kura ya maoni ya Sudan ya Kusini

Kura ya Maoni itakayopigwa na wakaazi wa Sudan ya Kusini Januari 9 mwakani imezua wasiwasi katika jumuiya ya kimataifa kuhusu hatima ya nchi ya Sudan

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, akipiga kura katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mjini Khartoum, Aprili, 2010. (AP Photo/Amr Nabil)

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, akipiga kura katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mjini Khartoum, Aprili, 2010. (AP Photo/Amr Nabil)

Raia wenye utajiri wa mafuta katika ardhi yao, lakini walilofukarishwa kutokana na miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, sasa wanakwenda kupiga kura ya maoni kuamua hatima ya eneo lao la Sudan ya Kusini. Lakini kama ulivyo uwezekano wa sehemu hii ya Sudan kuamua kujitenga, ndivyo ulivyo uwezekano wa kutokufanikiwa kwa kura hii. Hiyo ndiyo khofu ya jamii ya kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amenukuliwa na Shirika la Habari la AFP akisema kwamba suala la Sudan ni miongoni mwa "vipaumbele" vyake "vya juu kabisa." Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kijiografia Sudan ni taifa kubwa linalopakana na nchi zenye migogoro, ukiacha mbali migogoro iliyomo ndani yake yenyewe. Sudan inapakana na karibuni nchi zote za Mashariki na Kati ya Afrika zenye migogoro: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia, Uganda na Chad.

Kiuchumi, nchi hii inazalisha mafuta kwa wingi na kwa sasa mteja wake mkubwa ni China, ila kutokana na umuhimu wa nishati hiyo duniani, uwezekano wa mataifa mengine kuinyemelea ni mkubwa.

Rais wa Sudan ya Kusini, Salva Kiir.

Rais wa Sudan ya Kusini, Salva Kiir.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton, ameifanisha hali ya sasa ya Sudan na "bomu linalosubiri kupasuka". Tayari Ikulu ya Marekani imeshatoa msimamo wake kuhusiana na kura hii ya maoni ikisema uhusiano baina ya nchi hiyo na Sudan, utategemea zaidi na namna Khartoum itakavyotekeleza wajibu wake kwenye kura ya maoni ya Sudan ya Kusini. Hadi sasa kasi ya matayarisho ya kura hiyo ni ndogo. Kwa mfano, ikiwa imebakia miezi isiyofika minne, bado usajili wa wapiga kura haujafanyika hadi sasa.

Ingawa mara kadhaa Rais wa Sudan, Omar Al-Bashir, amesema atakubaliana na maamuzi yoyote yatakayotolewa na Wasudan ya Kusini kupitia kura hii, kauli hii inatiliwa shaka. Wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa pia ni kwamba, kama kura hii haikufanyika kama ilivyopangwa, viongozi wa Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan ya Kusini, SPLM, wanaweza kutangaza kujitenga kutoka Sudan ya Kaskazini na hivyo kuanzisha upya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kesho, Ijumaa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kwenye kikao maalum kuhusiana na kura ya maoni ya Sudan, ambapo Rais wa Marekani, Barack Obama, ni miongoni wa washiriki wa kikao hicho ambacho kitakachotoa msukumo wa kusaidia kufanyika kwa kura hiyo.

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amemteua Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, kuongoza jopo litakaloangalia mwenendo wa kura hii ya maoni. Marekani, Uingereza na Norway zimeshawaandikia barua viongozi wa Sudan kuwataka wahakikishe kuwa kura hii inafanyika kwa wakati na katika misingi ya uwazi na ya kidemokrasia.

Mwandishi: Mohamed Khelef/

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com