Jumuiya ya ECOWAS yamtambua Ouattara kama rais wa Cote d´Ivoire | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 08.12.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Jumuiya ya ECOWAS yamtambua Ouattara kama rais wa Cote d´Ivoire

Viongozi wa nchi na serikali za Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS wamemtambua Alassane Ouattara kama Rais aliyechaguliwa nchini Cote d'Ivoire na kumtaka rais Laurent Gbagbo kukubali kushindwa

default

Alassane Ouattara atambuliwa na jumuiya ya ECOWAS kama rais mpya wa Cote d´Ivoire

Baada ya mkutano wa dharura uliohudhuriwa na viongozi wa mataifa ya kanda hiyo, uliofanyika Abuja Nigeria, Jumuiya hiyo ya ECOWAS imemuongezea mbinyo zaidi Bwana Gbagbo kwa kuisimamisha nchi hiyo kujihusisha na kundi hilo.

Aidha, Rais wa muda wa ECOWAS, Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameonya dhidi ya juhudi za kuzuia makubaliano hayo, kama ilivyotokea nchini Kenya na Zimbabwe.

Awali Bwana Gbagbo alikataa kutekeleza matakwa ya kimataifa, ya kumtaka kukubali kushindwa na badala yake kutangaza baraza lake la mawaziri, ikiwa ni siku mbili tu baada ya mpinzani wake Alassane Ouattara kutangaza pia serikali yake, chini ya ulinzi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa. Jana Gbagbo alifanya kikao cha kwanza cha baraza lake la mawaziri.

Mabishano yaliyozuka kufuatia matokeo ya uchaguzi wa rais nchini humo mwezi uliopita katika nchi hiyo iliyo maarufu kwa zao la kakao, yamezidisha hatari ya kutokea tena ghasia katika taifa hilo ambalo bado limegawanyika baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002 na 2003, hali iliyosababisha pia Umoja wa Mataifa kuondoa baadhi ya wafanyakazi wake.

Kwa mujibu wa shirika la Kimataifa la Msalaba mwekundu, mapigano kati ya majeshi ya ulinzi na kati ya wafuasi wanaopingana wa viongozi hao yamesababisha vifo vya watu 28 na wengine 280 kujeruhiwa tangu Novemba 26.

Wakati huo huo, Katika Umoja wa mataifa wanadiplomasia wanasema kuwa Urusi imeipinga taarifa iliyotolewa ya kumtambua Alassane Ouattara kama Rais wa Cote d'Ivoire.

Wanadiplomasia wamearifu kuwa baada ya mazungumzo ya faragha yaliyodumu kwa takriban saa tano na nusu, mazungumzo hayo yaliahirishwa kwa siku kwa wajumbe wa Urusi kusema kwamba wanahitaji maelekezo zaidi kutoka Moscow.

Nafasi ya Urusi ni nguzo kubwa kwa sababu taarifa za Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa lazima ipitishwe na wote bila ya kupingwa, ikiwa na maana kuwa mwanachama yeyote akipinga maamuzi yaliyofikiwa atazuia hatua hiyo.

Susan Rice

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa,Susan Rice, ambaye kwa sasa ndiye rais wa mwezi wa baraza hilo amesema ana matumaini kuwa mjadala huo utaendelea leo.

Kwa upande wake, mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Afrika magharibi Y J Chio amethibitisha kuwa Ouattara ndiye mshindi, ambapo alilifahamisha baraza la usalama pia kwamba matokeo ya uchaguzi yalikuwa wazi na kwamba kulikuwa na mshindi mmoja tu.

Awali akithibitisha hilo alisema, '' Matokeo yamethibitisha tena Bwana Ouattara kuwa ni mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Cote d'Ivoire.''

Kuidhinishwa huko kwa Bwana Ouattara na Umoja wa mataifa kumemfanya Bwana Gbagbo kuwa na wafuasi wachache kimataifa baada ya jumuia ya ECOWAS pia kumtambua Ouattara.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, reuters)

Mhariri:Josephat Charo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com