Julius Yego aweka historia ya kurusha mkuki | Michezo | DW | 27.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Julius Yego aweka historia ya kurusha mkuki

Kenya imeshinda dhahabu nyengine mbili katika mashindano ya riadha yanayoendelea mjini Beijing China. Kenya sasa inaongoza msimamo wa medali ikiwa na dhahabu sita

Mrusha mkuki wa Kenya Julius Yego alirusha umbali wa 92.72 na kupata ushindi mbele ya aliyekuwa bingwa wa Afrika Abdelrahman el Sayid wa Misri.

Ni urefu ambao haujawahi kufikishwa duniani tangu Jan Zelezny aliyeweka rekodi ya 98.48 katika mashindano ya dunia mwaka 2001. Ni Zelezny na Aki Parviainen wa Finland waliorusha zaidi ya Yego.

Bingwa wa zamani wa kurusha mkuki barani Afrika Ihab Abdelrahman El Sayed wa Misri alijipatia medali ya fedha kwa kurusha umbali wa 88.99.

Wakati huo huo Mkenya mwengine Hyvin Jepkemoi alihimili ushindani mkubwa kutoka kwa wanariadha wawili na kushinda mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa upande wa wanawake. Jepkemoi alimpiku mwanariadha wa Tunisia Habiba Ghribi kwa kuongeza kasi katika mita 30 za mwisho.

Mjerumani Gesa Krause alipata medali ya shaba baada ya kumaliza wa tatu huku bingwa wa Olimpiki na mshindi wa medali ya shaba Sofia Assefa wa Ethiopia akichukua nafasi ya nne.

Kenya sasa imeshinda dhahabu zote mbili katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji upande wa wanaume na wanawake baada ya Ezekiel Kemboi kushinda dhahabu siku ya jumanne.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef